SERIKALI imezitaka Taasisi za Elimu kutoa Elimu itakayowawezesha wahitimu kuweza kujiajiri na siyo kusubiri kuajiriwa.

Akifungua Kongamano la Kitaaluma la kumuenzi Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere lililoandaliwa na Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia Dkt Francis Michael amesema Elimu bora ndiyo itakayowezesha watanzania kuondokana na Ujinga, Umasikini na Maradhi.

Dkt Michael amesema katika kuenzi maono ya Baba wa Taifa,   Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia  imeona umuhimu wa kuboresha Mitaala na Sera ili kuwajenga vijana katika misingi ya kujitegemea.

"Mitaala ya sasa inamuandaa kijana kukua katika misingi ya kuajiriwa jambo ambalo serikali imekuwa ikipambana ili kuondokana na dhana hiyo na kwamba kwa sasa maoni mbalimbali yanaendelea kupokelewa kutoka kwa wadau yanaendelea kutolewa," alisema Dkt Michael.

Dkt Michael amekipongeza Chuo kwa kuandaa kongamano na kuendelea kumuenzi baba wa Taifa, na kusema kuwa Elimu bora ndiyo mbegu ya Maendeleo itakayowezesha kuchangia katika Maendeleo.


Kwa upande wake Mkuu wa Chuo chá Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere Prof. Shadrack Mwakalila amesema Chuo kinapambana na ujinga siyo kwa kufundisha tu bali kuangalia changamoto zinazoikabili jamii kwa kufanya tafiti mbalimbali zinazoleta matokeo katika jamii.

Alisema kongamano hili limejikita kupambana na maadui watatu ambao ni Ujinga, Umasikini na Maradhi na kuwa katika kongamano hilo la siku mbili mada mbalimbali zilizofanyiwa utafiti zitawasilishwa na kupatiwa Ufumbuzi.

Prof Mwakalila alisema Kongamano hilo la siku mbili linaongozwa na kauli mbiu inayosema” Mchango wa mwalimu Nyerere katika kuimarisha Ustawi wa Maendeleo ya Watanzania.Katika hotuba yake Prof Mwakalila alielezea historia ya Chuo hicho kuwa kilianzishwa kutokana na Chuo cha Kivukoni ambacho kilianzishwa rasmi tarehe 29 Julai 1961. 


Prof Mwakalila amesema Chuo hiki kimepewa jina la Mwalimu Nyerere kwa lengo la kumuenzi Baba wa Taifa ambaye alifanya kazi kubwa ya ukombozi wa Taifa letu, Ukombozi wa Afrika na kuwatetea wanyonge popote duniani.

 Imetolewa na:

Kitengo cha Habari na MahusianoChuo Cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere

Share To:

Post A Comment: