Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki (wa tatu kutoka kulia) akikata utepe kuashiria  ishara ya uzinduzi wa shamba la uzalishaji kuku wazazi lililopo kwenye Wilaya ya Siha mkoani Kilimanjaro katikahafla iliyofanyika jana Septemba 2, 2022.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki akizungumza na wananchi pamoja na watendaji wa shamba la uzalishaji wa kuku wazazi (Aviagen East Africa) ( hawapo pichani) wakati wa uzinduzi wa shamba hilo uliofanyika kwenye Wilaya ya Siha mkoani Kilimanjaro, jana Septemba 2, 2022. 

 

Na Mwandishi Wetu, Kilimanjaro

 

WAZIRI wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki amewataka  wawekezaji  kutoka ndani na nje ya nchi  kuwekeza katika sekta ya mifugo huku akisisitiza  kuwa mazingira ya uwekezaji kwa sasa hapa nchini ni salama chini ya Uongozi wa  Rais  wa jamuhuri wa muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan.

Aliyasema hayo  katika uzinduzi wa shamba la  kuku wazazi  la kuzalisha  babu na bibi (grand parent stock) uliofanyika wilayani siha Mkoani Kilimanjaro jana Septemba 2, 2022.

Alisema uzinduzi wa mradi huo uliogharimu Dola za kimarekani Milioni 15 utasaidia kupanua sekta ya kuku nchini pamoja na kuongeza lishe  kwa watanzania kutokana na  bidhaa zitokanazo na kuku.

"Sisi kama Wizara tunapongeza uwekezaji huu utakaosaidia kupanua sekta ya kuku nchini, utachechemua biashara na kuongeza mzunguko wa fedha, hivyo tunamshukuru Rais  Samia kwa kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji   hapa nchini na matokeo yake tunayaona," alisema.

Aliongeza kwa  kusema kuwa  kuku watakaozalishwa katika shamba hilo  watauzwa maeneo mbalimbali hapa nchini pamoja na nje ya nchi hali itakayopelekea ongezeko la kipato kwa mtu mmoja moja na taifa kwa ujumla.

Aidha aliwataka wananchi wa Wilaya ya  Siha kuwakumbatia wawekezaji wa shamba hilo lengo likiwa ni kunufaika na ufugaji huo ikiwa ni pamoja na kuuza vifaranga hao kwa nchi za jirani.

" Tumekuwa tukiagiza vifaranga wazazi kutoka nje na kutumia fedha nyingi, uwepo wa mradi huu utapunguza matumizi ya fedha za kigeni na kukuza uchumi wa nchi kwa kuwa tutakuwa tunazalisha  hapa hapa nchi, aliongeza.

Pia, alifafanua kuwa uwepo wa wawekezaji hao utasaidia kutekeleza adhma ya serikali ya kutengeneza  ajira zaidi ya  milioni 8 ifikapo 2025 pamoja na kuongeza kipato cha mtu mmoja mmoja.

Akielezea mradi huo Mwenyekiti wa Kampuni ya Aviagen Afrika Mashariki Bw. Kester lyaruu alisema kuwepo kwa mradi huo kutachangia kuleta usalama wa chakula pamoja na kuzuia uingizwaji wa vifaranga visivyo salama kutoka nje ya nchi.

"Mradi huu utasaidia uchumi wa nchi na kuongeza lishe kwa wananchi wa kawaida ambao wataweza kupata vifaranga hao kwa bei nafuu" alisema Lyaruu.

Aidha Mkuu wa Wilaya ya Siha Mhe. Thomas Apson alisema mradi huo wa kuku ni wa kuzalisha vifaranga wazazi mababu na mabibi watakaoendelea kuzalisha kuku wengi zaidi.

Mwananchi kutoka Wilaya ya Siha Bi. Witness Philemon alisema, wanapata ajira mbalimbali kutokana na uwekezaji huo na kuiomba Serikali kuanzisha miradi ya ufugaji kuku katika vijiji na vitongoji Ili kusaidia kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.

Share To:

dottomwaibale

Post A Comment: