Na Mwandishi Wetu, Bumbuli


WANANCHI wa kijiji cha Kwesine kilichopo kata ya Baga, tarafa ya Mgwashi, Halmashauri ya Bumbuli, wilaya Lushoto, wameiomba serikali iwasaidie kutua mzigo wa michango wanayochanga  kujenga zahanati na shule ya Sekondari.


Sanjari na ombi hilo, pia wananchi wa kijiji hicho wamewaomba viongozi wao, wawape maelezo ya fedha walizokusanya tangu waanze michango miaka minne iliyopita.


Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi, kijijini hapo, baadhi ya wananchi walisema hadi sasa majengo waliyojenga ya zahanati na sekondari yamefikia hatua ya kumalizia lakini wanahisi nguvu zao zimeishia hapo.


"Mfano zahanati tumeshaanza kuiezeka lakini kuna bati zimefemea na sekondari pia tumeezeka vyumba viwili na viwili vimebaki," alisema Bashiru Ashrafu.


Mwananchi mwingine Fadhila Idd Sheshe, alisema waliamua kuingia kwenye ujenzi wa zahanati na sekondari kutokana na watoto wao kukosa huduma hizo ikiwemo huduma ya afya ya mama na mtoto.


"Watoto wanaosoma sekondari ya kata ya Baga, kutoka hapa hadi Baga ni kilomita 7 kwenda na kurudi watoto wetu wanatembea umbali mrefu wa kilometa 14, wanachoka sana kiukweli sasa serikali itusaidie, umuhimu wa hizi huduma ni mkubwa sana," alisema Asha Malika na kuongeza,


"Sisi wanawake tukitaka kwenda kwenye zahanati lazima twende Baga, Mbelei au Masange kote huko ni kilomita 5 wakati mwingine akina mama wanajifungulia njiani hasa kipindi cha mvua,".


Mwenyekiti wa kijiji hicho Paulo Danga, alisema ni kweli wananchi wamechangishwa fedha kujenga zahanati na sekondari kati ya shilingi 5,000 hadi 10,000 kwa kila mtu mwenye uwezo wa kufanya kazi baada ya kijiji kuamua kuanzisha miradi hiyo miwili kusaidia na kusogeza huduma karibu na wananchi wapatao 2,290 waliopo katika kijiji hicho chenye kaya 528 na vitongoji tisa.


"Kijiji chetu kimesajilia mwaka 1975, hadi sasa kina zaidi ya miaka 47 lakini hatuna zahanati wala shule ya sekondari na watoto wetu wanasoma mbali na akina mama wajawazito wanapata changamoto wakati mwingine wanajifungulia njiani," alisema Mwenyekiti huyo.


Mtendaji wa kijiji hicho, Abdallah Kasimu alisema hadi sasa zahanati imetumia kiasi cha shilingi milioni 38 na  sekondari imetumia kiasi cha shilingi milioni 33.7.


Diwani wa kata ya Baga Ramadhani Kingazi, alikiri wananchi kuchangishwa lakini akasema kwamba mbunge wao January Makamba amechangia kwa kiasi kikubwa hadi majengo hayo yamefikia hapo ikiwemo kutoa fedha kutoka mifukoni kwake na mfuko wa jimbo.


"Zahanati bado bati 70 tumalizie kupaua na kupata saruji kwa ajili ya kupiga plasta, kusakafia vyumba, kuweka madirisha na milango, mbunge nimeongea naye amesema atamalizia hizo bati" alisema.


Menyekiti wa halmashauri hiyo Amir Shehiza alipoulizwa alisema kwambwa zahanati na sekondari zilizopo katika kijiji hicho wataziingiza katika bajeti ya mwaka huu na kwamba watamaliza ili wananchi wasogesewe huduma karibu kama dhima ya serikali.


Alisema kila mwaka wamekuwa wakizisaidia zahanati tatu na kwa mwaka jana walimalizia zahanati za Nkongoi, Kwadoye na Kwemkomole kwa bajeti ya shilingi milioni 150 wanazoletewa na serikali kila mwaka.


Mkurugenzi wa halmashauri ya Bumbuli George Haule alisema watasaidia majengo hayo katika bajeti ya mwaka huu na akaahidi kwenda kutazama changamoto hizo ili waweze kuyamaliza mjengo hayo huku akikiri watoto kusoma umbali mrefu zaidi.

Mwisho

Share To:

Post A Comment: