HALMASHAURI ya Jiji la Dodoma imepongezwa kwa kusimamia maazimio ya vikao yanayolenga kutatua changamoto zinazoigusa jamii kwa kununua mitambo miwili ya kufungua barabara katika maeneo yaliyopimwa viwanja ili kuwarahisishia wananchi shughuli za ujenzi.


Pongezi hizo zilitolewa na Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Jabir Shekimweri kabla ya uzinduzi wa awali wa mitambo miwili kwa ajili ya ufunguzi wa barabara katika maeneo mbalimbali yaliyopimwa viwanja tukio lililofanyika katika kiwanda cha kuzalisha tofali za gharama nafuu Kata ya Kizota jijini Dodoma.

Shekimweri aliipongeza Halmashauri ya Jiji kwa kutekeleza maazimio ya vikao vya kisheria vinavyolenga kutatua changamoto zilizopo katika jamii. “Nawapongeza kwa uthubutu na kusimamia maazimio yenu ya vikao vya kisheria, Kamati ya Fedha na Utawala na Baraza la Madiwani ambao waliainisha umuhimu wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma kuwa na mitambo yake yenyewe kwa ajili ya kutekeleza miradi yake kwa gharama nafuu.

Na kuendeleza alama ambayo Jiji la Dodoma imejiwekea katika matumizi ya fedha za mapato ya ndani. Halmashauri ya Jiji la Dodoma ni miongoni mwa halmashauri chache nchini ambazo mapato yake ya ndani yanaacha alama. Tunafahamu mnafanya hayo kwa kuzingatia miongozo ya kibajeti, lakini sisi Jiji la Dodoma huu ni utashi wetu wa kujihoji na kuacha alama kubwa kwa bajeti tunayoacha katika mwaka wa fedha husika” alisema Shekimweri kwa kujiamini.

Akiongelea umuhimu wa mitambo hiyo kwa Halmashauri ya Jiji la Dodoma na wananchi kwa ujumla, alisema kuwa mitambo hiyo itasaidia kufungua barabara katika maeneo yaliyopimwa viwanja. “Mitambo hii pamoja na kufungua barabara pia itasaidia kuweka mandhari ya jiji vizuri na kuongeza thamani ya maeneo husika. Barabara zikifunguliwa zitasaidia kupunguza gharama za uendeshaji kwa sababu wananchi wanashindwa kuendeleza viwanja vyao kutokana na kutokufikika. Hivyo, mitambo hii ni suluhisho kwa wananchi” alisema Shekimweri.

Akiwasilisha taarifa ya ununuzi wa mitambo miwili kwa Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Joseph Mafuru alisema kuwa mitambo hiyo inaenda kutatua migogoro inayoendelea katika jiji hilo ya wananchi kujenga maeneo ya barabara kutokana na kutokuwa na barabara zilizofunguliwa. Alisema kuwa halmashauri imepima zaidi ya viwanja 700,000 kwa upimaji shirikishi, utwaaji na urasimishaji. “Kilio cha wananchi kimekuwa ni baada ya kupima viwanja lini barabara zitafunguliwa na kuchongwa. Halmashauri ina barabara zenye urefu wa kilometa 1,768 zinazotakiwa kufunguliwa” alisema Mkurugenzi Mafuru.

Akiongelea gharama za ununuzi wa mitambo hiyo, Mkurugenzi Mafuru alisema kuwa mitambo hiyo imegharimu shilingi 1,818,716,3000. Aliitaja mitambo hiyo kuwa ni Greda (140K) limegharimu shilingi milioni 943.5 na Buldoza (D6) limegharimu shilingi milioni 863.33 na usafiri kutoka Dar es salaam hadi Dodoma uligharimu shilingi 11,800,000.

Mkurugenzi huyo aliyataja maeneo ambayo yanauhitaji mkubwa wa kufungua Barabara kuwa ni Ndachi Mnadani, Michese, Nala Lugala, Zuzu, Iyumbu, Ngh’ong’ona, Mkonze, Makutopora, Ntyuka, Nala Chihoni, Mbwanga, Veyula, Msalato, Hombolo na Miyuji.

Kwa upande wa Mbunge wa Jimbo la Dodoma mjini, Anthony Mavunde alilishukuru Baraza la Madiwani na Menejimenti ya jiji kwa kuona umuhimu wa kuwa na mitambo hiyo. “Nachukua nafasi hii kupongeza hatua hii kubwa iliyofikiwa. Naamini wananchi wanakwenda kutatuliwa migogoro yao na maeneo yaliyokuwa hayafikiki, sasa yanakwenda kufikika” alisema Mavunde.

Akitoa shukrani kwa mgeni rasmi, Naibu Meya wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Jamal Ngalya alimhakikishia Mkuu wa Wilaya ya Dodoma kuwa usimamizi mzuri wa Baraza la Madiwani na Menejimenti kwa mitambo hiyo. “Mheshimiwa mkuu wa wilaya mitambo hii tutaisimamia vizuri na kuratibu matumizi yake. Lakini Mhehsimiwa mkuu wa wilaya tunakupongeza na wewe kwa usimamizi wako madhubuti” alisema Ngalya.

Share To:

Post A Comment: