KAMPENI  ya  kitaifa ya usafi wa mazingira na kuongezeka kwa wananchi wanaopata  huduma ya maji kumetajwa kuimarisha afya ya Watanzania kwa kupunguza kwa kiasi kikubwa  magonjwa ya mlipuko.

Mwakilishi wa Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Dk Saitore Laizer, alisema hayo mwishoni mwa wiki wakati wa uzinduzi wa Programu ya Maendeleo ya Sekta  ya Maji awamu wa tatu (WSDP 111) inayotarajia kugharimu dola bilioni 6.5.

”Kiwango cha huduma ya maji katika maeneo ya huduma ya afya kimeimarika hivyo huduma za afya kuwa bora na salama,” alisema Dk Laizer na kuongeza kuwa kumekuwa na ongezeko kubwa la kaya zinazotumia vyoo na kunawia mikono kwa kutumia maji tiririka.

Aidha vituo vipya vya afya 1,534 vimefikiwa na huduma ya maji.

“Hata vyumba vya kujifungulia vina huduma ya maji. Hili litasaidia kupunguza maambukizi kutoka  kwa mama kwenda kwa mtoto wakati wa kujifungua na hivyo kupunguza  vifo vya watoto wachanga,” alisema.

Alisema kuwa katika mpango wa tatu wa programu ya maji wanategemea  kuimarika kwa afya ya jamii kwani   kila kaya, ifikapo 2025 inatarajiwa itakuwa na choo bora.

Vile vile serikali inategemea vituo vipya 3,500 vitafikiwa na  huduma ya maji hasa vijijini hatua itakayoongeza usafi katika maeneo ya umma , magulio na masoko. “Tuko tayari kwa ajili ya utekelezaji wa mpango wa tatu,” alisema.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa  James Mdoe alisema wamekuwa wadau muhimu katika programu hiyo kwa kujenga vyoo bora, vifaa vya kunawia mikono  kwa shule za msingi na sekondari.

Alisema katika utekelezaji wa programu hiyo awamu ya pili, zilihudumiwa shule za msingi 3,046 na sekondari 716. Katika awamu ya tatu, zitafikiwa shule za msingi 2,500 na sekondari  1,400. Pia vitajengwa  vyoo bora  na  kuwezesha upatikanaji maji na vifaa bora vya kunawia mikono

Mkuu wa Kitengo cha Uratibu Wizara ya Maji,  Remigius Mazigwa akitoa taarifa kuhusu WSDP III wakati wa uzinduzi huo alisema kuwa maabara nyingi za maji zimepata ithibati.

Alisema utekelezaji wa mpango wa pili ulikuwa na changamoto ikiwamo  kupungua kwa raslimali maji kutokana na mito mingi kukauka kunakochangiwa na mabadiliko ya tabia nchi.

“Fedha zilizotolewa katika awamu ya pili ni asilimia 37 tu  na kuna umuhimu wa kuongeza fedha ili programu ya tatu itekelezwe kwa ufanisi,” alisema. Alisema kuwa awamu ya tatu inatarajiwa kutumia dola bilioni 6.5.

“Waliangalia tathimini iliyofanyika na kazi  iliyobaki , fedha zikipatikana tutafika mbali,” alisema.

Mwakilishi wa wadau wa maendeleo, Ruth Kennedy Walker kutoka Benki ya Dunia, aliipongeza serikali kwa jitihada zinazofanyika kuhakikisha changamoto za upatikanaji wa majisafi na salama zinapatiwa ufumbuzi. Alisema benki iko tayari kuendeleza ushirikiano huo.

Ruth  alipongeza serikali kwa jitihada zinazofanyika kuhakikisha changamoto za upatikanaji wa maji safi na salama zinapatiwa ufumbuzi.

Akizungumza kwenye uzinduzi huo, Waziri wa Maji Jumaa Aweso alisema gharama ya utekelezaji wa programu hiyo inakadiriwa kuwa Dola za Marekani bilioni 6.46.

Programu inalenga kufanikisha utekelezaji wa miradi ya usimamizi na uendelezaji rasilimali za maji, upatikanaji wa majisafi na salama na miradi ya usafi wa mazingira nchini.

Alisema baada ya kukamilika kwa programu ya maendeleo ya  sekta ya maji awamu ya kwanza na ya pili, wizara inajivunia mafanikio makubwa ambayo ni pamoja na maboresho katika usimamizi na uendelezaji wa rasilimali za maji.

Usimamizi huo ni pamoja na kuanzishwa kwa bodi tisa za maji za mabonde, maabara saba kati ya 17 za ubora wa maji kupewa vyeti vya ithibati, kuimarika kwa kiwango cha huduma ya maji vijijini hadi kufikia asilimia 72.3.

Share To:

Post A Comment: