Kassim Nyaki, NCAA

Uboreshaji wa huduma za kijamii katika Kijiji cha Msomera Handeni Mkoani Tanga umeendelea kuvutia wananchi wanaoishi eneo la Hifadhi ya Ngorongoro kujiandikisha kwa wingi ili kuhama kwa hiari yao kwa ajili ya kupisha shughuli za uhifadhi.

Akiwaaga wananchi ambao ni kundi la pili awamu ya pili lenye kaya 28 zenye watu 148 pamoja na mifugo takribani 718 wanaohamia Msomera, Waziri wa maliasili na Utalii Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana ameelezea kuwa hamasa ya wananchi wanaoishi Ngorongoro kuhamia Kijiji cha Msomera imeongezeka kutokana na jitihada za Serikali kuboresha huduma zote muhimu za kijamii.

“Hamasa tunayoiona ya wananchi kuendelea kujiandikisha kuhamia Kijiji cha Msomera inatokana na Habari chanya wanazopata kwa waliotangulia kuhusu Serikali kuboresha huduma za kijamii kama maji, afya, shule, majosho, barabara, malambo, malisho na uwepo wa fursa za kiuchumi kama kilimo, biashara, uwekezaji na ujenzi wa nyumba bora na za kudumu ” ameongeza Mhe. Balozi Chana.

Naibu kamishna wa Uhifadhi NCAA Dkt. Christopher Timbuka ameleeza kuwa hadi kufikia tarehe 25 Agosti, 2022 jumla ya Kaya 1002 zenye jumla ya watu 5,382 zimejiandikisha kuhama kwa hiari.

Amebainisha kuwa kati ya kaya hizo zilizojiandikisha, kaya 624 zenye watu 3,323 tayari zimehakikiwa na kufanyiwa uthamini. Kati ya kaya hizo zilizofanyiwa uhakiki na uthamini, jumla ya kaya 131 zenye watu 651 na jumla ya Mifugo 2,392 zimeshahamia Kijiji cha Msomera.

Dkt. Timbuka amebainisha kuwa kuendelea kujitokeza wananchi wengi kuhama katika eneo la Hifadhi ya Ngorongoro zinatokana na jitihada za Serikali kuwaelemisha wananchi juu wa uwepo wa fursa za uwepo wa maisha bora ambayo ni rahisi kwao kuzifanya nje ya eneo la Hifadhi.

Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro Mhe. Raymond Mwangala ameeleza uongozi wa Mkoa wa Arusha na Wilaya ya Ngorongoro utaendelea kutoa ushirikiano na usalama kwa wananchi wote ambao wanaendelea kujiandikisha kwa hiari kwenda Kijiji cha Msomera kwa ajili ya kupisha shughuli za Uhifadhi ndani ya eneo la Hifadhi ya Ngorongoro.

Wananchi waliojiandikisha kwa hiari kuhama kutoka eneo la Hifadhi ya Ngorongoro kwenda Kijiji cha Msomera wanapata fursa ya kupewa nyumba bora yenye eneo la ekari 2.5, hati ya nyumba na shamba, huduma bora za afya, elimu, nishati ya umeme, maji, barabara na kupewa eneo lenye ekari 5 kwa ajili ya shughuli za kijamii.













Share To:

Post A Comment: