Na John Walter-Manyara

Mkuu wa mkoa wa Manyara, Charles Makongoro Nyerere amesema atamkumbuka mwenyekiti wa TLP Agustino Mrema  kwa mchango wake katika mageuzi ya siasa, uzalendo,Upendo na kujituma kuwatumikia wananchi. 

Ameeleza kuwa marehemu Agustino Mrema alikua kama kaka yake, wakishirikiana kwenye mambo mbalimbali tangu akiwa katika chama cha mapinduzi na kutumikia kama Mbunge lakini pia Waziri, na hata baada ya kutoka CCM kwa nia ya kutaka kulitumikia Taifa kama Rais kupitia chama chake cha TLP.

Makongoro ameongeza kuwa hata namna ya kuzungumza kwenye majukwaa alijifunza kutoka kwa kiongozi huyo ambaye aliweza kuzungumza na wananchi na kukubalika.

"Sitoweza kusahau  nilvyojifunza kutoka kwa marehemu Mrema namna ya kuongea na wananchi kwenye majukwaa, wakati huo mimi nikiwa kama meneja wake wa kampeni za kugombea Urais" alisema Nyerere. 

"Tuliishi kama ndugu, nakumbuka hata kipindi cha msiba wa mke wa mzee Mrema, Mama Rose alinipa taarifa, nikafika tukashirikiana na hata alipotaka kuoa tena alinialika" aliongeza Makongoro.

Nyerere amesema licha ya majukumu ya kiserikali yanayowataka wakuu wa mikoa wote kuwepo katika maeneo yao ya kazi mpaka tarehe 29, atajitahidi kwa kadiri ya uwezo wake ili aweze kushiriki katika Ibada ya kumsitiri marehemu Mrema katika nyumba yake ya milele hapo kesho, Agosti 25 nyumbani kwake, Kiraracha mkoani Kilimanjaro.

Augustino Mrema (77) anatarajiwa kuzikwa  Alhamisi agosti 25 kijijni kwake Kiraracha mkoani Kilimanjaro.

Share To:

Post A Comment: