Mkuu wa Wilaya ya Njombe mkoani Njombe Kissa Kasongwa (katikati) akiwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Etv na Efm Redio, Majizzo (wa pili kushoto) kwenye Tamasha la Mziki Mnene lililofanyika Agosti 13, 2022 Uwanja wa Sabasaba mjini Njombe kwa ajili ya uhamasishaji wa chanjo ya UVIKO 19. Wengine ni Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Njombe Filoteus Mligo (wa pili kulia), Mganga Mkuu wa Mkoa wa Njombe Dkt. Zabron Masatu (kulia) na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Njombe Kuruthum Sadick (kushoto). (Picha na Yusuph Mussa)
Wananchi wakiwa wamefurika kwenye Tamasha la Mziki Mnene lililofanyika Agosti 13, 2022  Uwanja wa Sabasaba mjini Njombe kwa ajili ya uhamasishaji wa chanjo ya UVIKO 19. (Picha na Yusuph Mussa).
 Wananchi wakiwa wamefurika kwenye Tamasha la Mziki Mnene lililofanyika Agosti 13, 2022  Uwanja wa Sabasaba mjini Njombe kwa ajili ya uhamasishaji wa chanjo ya UVIKO 19. (Picha na Yusuph Mussa).



Na Yusuph Mussa, Njombe

MKUU wa Wilaya ya Njombe mkoani Njombe Kissa Kasongwa amesema wapo kwenye jitihada za kuongeza idadi ya watu wanaochanja chanjo ya UVIKO 19 kwenye wilaya hiyo, na ndiyo maana wanafanya jitihada mbalimbali ikiwemo kuandaa matamasha.

Aliyasema hayo Agosti 13, 2022 kwenye tamasha la Mziki Mnene lililoratibiwa na Efm Redio kutoka Dar es Salaam na Ofisi ya Mganga Mkuu wa Mkoa wa Njombe na kufadhiliwa na Epic/ FHI 360 kwa ajili kuhamasisha wananchi wachanje chanjo ya UVIKO 19, ambalo tamasha hilo lilifanyika Uwanja wa Sabasaba mjini Njombe.

"Tupo kwenye jitihada za kuongeza idadi ya wananchi wanaochanja chanjo ya UVIKO 19. Nia yetu ni kuona asilimia 70 ya wananchi wa Wilaya ya Njombe wanakuwa wamechanja. Wataalamu wanasema, kama asilimia 70 wataweza kuchanja, itakuwa ni kinga kwa wengine" alisema Kasongwa wakati anazungumza na wanahabari pembeni ya tamasha hilo.

Akizungumza na wananchi kwenye tamasha hilo, Kasongwa aliwaasa wananchi kujitokeza kwa hiari yao na kuchanja chanjo ya UVIKO 19 ili waendelee kuwa salama, na kuendelea na shughuli zao za kila siku kwa amani.

'Ujanja ni kuchanja. Kuchanja sio suala la mzaha. Rais wetu Mama Samia Suluhu Hassan ametutaka tuchanje kwa hiari yetu ili tuwe salama. Hata Shirika la Afya Duniani (WHO) linatutaka tuchanje. Tukichanja tutaushi, ila tukiacha kuchanja tutakufa. Tuhakikishe tunachanja na kuepukana na ugonjwa huu wa hatari" alisema Kasongwa akiwa amemuwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Njombe Anthony Mtaka kwenye tamasha hilo.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi mara baada ya zoezi hilo la uhamasishaji wa chanjo ya UVIKO 19 kukamilika, Mratibu wa Chanjo Halmashauri ya Mji Njombe Simon Ngassa, alisema watu waliojitokeza kuchanja kwenye tamasha hilo ni 4,563, ambapo wanaume ni 1,954 na wanawake 2,609.

"Lengo ni kuchanja watu 98,396, ambao Ni asilimia 70 ya watu wenye umri wa miaka zaidi ya 18.. Tulianza kuchanja Agosti 3, 2021, na hadi Agosti 13, 2022 tumechanja jumla ya watu  92,422 sawa na asilimia  93.

"Dira yetu ni kufikia lengo la asilimia 100 ifikapo Septemba 30 mwaka huu 2022. Kwa kushirikiana na wadau wetu FHI360,  na wadau mbalimbali kwa pamoja na mikakati ya hamasa ya matamasha makubwa, na ushirikiano wa  DC (Kasongwa) na Mbunge (Deo Mwanyika- Njombe Mjini) katika ziara ya kijiji kwa kijiji kuhamasisha chanjo kwa wananchi" alisema Ngassa.

MWISHO.
Share To:

TANGA RAHA BLOG

Post A Comment: