Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini IGP Simon Sirro akisaini Kitabu cha Wageni mara baada ya kukamilisha ziara yake kwenye Banda la Maonesho la TCRA katika viwanja vya Maonesho ya Biashara-SabaSaba barabara ya Kilwa jijini Dar es salaam. Anaeshuhudia ni Afisa Mwandamizi Mkuu wa Mawasiliano-TCRA, Semu Sauli Mwakyanjala. Katika ziara yake Sirro alitoa mwito kwa TCRA kuendeleza kazi nzuri ya kutoa elimu kwa umma kuhusu matumizi salama ya mtandao. Picha na TCRA
Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini IGP Simon Sirro katika Mahojiano na Afisa Mwandamizi Mkuu wa Mawasiliano-TCRA, Semu Sauli Mwakyanjala kwenye banda la maonesho-SabaSaba barabara ya Kilwa jijini Dar es salaam, ambapo alielezea azma ya Jeshi la Polisi nchini kuendeleza ushirikiano na Mamlaka ya Mawasiliano katika kuhakikisha inatokomeza uhalifu mtandaoni. IGP Sirro alionya kwamba hakuna atakaetenda jinai mtandaoni asipatikane. Picha na TCRA.


Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini IGP Simon Sirro akiongozana na Afisa Mwandamizi Mkuu wa Mawasiliano-TCRA, Semu Sauli Mwakyanjala mara baada ya kupata maelezo ya Kazi za TCRA katika banda la Mamlaka hiyo katika viwanja vya Maonesho ya SabaSaba barabara ya Kilwa jijini Dar es salaam. Picha na TCRA.

***********************

Na Mwandishi Wetu

Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini IGP Simon Sirro amesisitiza kuwa, Jeshi la Polisi nchini litaimairisha zaidi ushirikiano baina yake na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), ili kuhakikisha watumiaji wa huduma za mawasiliano yakiwemo ya intaneti wanasalia salama wakati wote wanapotumia huduma hizo.

IGP Sirro alibainisha hayo wakati alipotembelea banda la maonesho la TCRA kwenye viwanja vya maonesho ya 46 ya biashara barabara ya Kilwa jijini Dar es salaam. Alibainisha kuwa hakuna mtu yeyote anaeweza kufanya uhalifu kwenye mtandao asipatikane.

“Hakuna namna unaweza kufanya uhalifu mtandaoni na usipatikane, na bahati mbaya utaadhirika kwa familia yako na jamii, kwa sababu utakamatwa tu, hivyo nawaasa sana watanzania wenzangu tujiepushe na utapeli mtandaoni” alionya IGP Sirro na kuongeza.

Alitoa mwito kwa TCRA kutoa elimu zaidi kwa watumiaji wa huduma za mawasiliano akibainisha kuwa hiyo ndiyo njia sahihi na muhimu zaidi ya kupunguza matukio ya uhalifu mtandaoni.

“TCRA najua wamejipanga na sisi Jeshi la Polisi pia tumejipanga,suala muhimu ambalo ningependa kuwashauri ni kwamba tuendelee kutoa elimu, tuna watu wetu wengine wanatenda uhalifu bila kujua kwamba ni uhalifu kwenye mtandao; hivyo elimu ni jambo la msingi sana”, alisisitiza IGP.

Awali, Afisa Mwandamizi Mkuu wa Mawasiliano na Uhusiano kwa Umma wa Mamlaka ya Mawasiliano Semu Sauli Mwakyanjala, akimkaribisha IGP Sirro bandani hapo alimweleza kwamba TCRA imeendelea na jitihada ya kutoa elimu kwa umma juu ya matumizi sahihi na salama ya huduma za Mawasiliano na kwamba imeweka utaratibu wa watumiaji huduma za Mawasiliano ya simu kutoa taarifa ya uhalifu kupitia namba maalum, sambamba na kuwataka watumiaji wote wa huduma za mawasiliano ya simu kuhakiki laini za simu zilizosajiliwa kwa namba za kitambulisho cha Taifa.

“Kamanda, TCRA tuna utaratibu unaomwezesha mtumiaji huduma za Mawasiliano ya simu kutoa taarifa ikiwa atapokea ujumbe au simu ya utapeli kw kutuma namba ya tapeli kwenda namba 15040, utaratibu huu tunautekeleza kwa ushirikiano na Jeshi la Polisi na Watoa Huduma umesaidia sana kupunguza ripoti za uhalifu” Semu alimweleza IGP.

Aliongeza kuwa, watumiaji wa huduma za mawasiliano wanapaswa kuhakiki usajili wa laini zao za simu kwa kubofya *106# ili kusalia salama akisisitiza kuwa hatua hiyo inamwezesha mtumiaji kufuta namba asiyoitambua kupitia wakala wa mtoa huduma.

Mbali na banda la TCRA Mkuu huyo wa Jeshi la Polisi nchini, alizuru mabanda kadhaa ya maonesho ya biashara likiwemo banda la Zanzibar linalojumuisha Taasisi za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na wajasiriamali wa visiwa vya karafuu.
Share To:

emmanuel mbatilo

Post A Comment: