Moses Mashalla,


Diwani wa viti maalumu (CCM) kata ya Mbuguni wilayani Meru mkoani Arusha,Husna Abdallah amesema kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Samia Suluhu Hassan ameonyesha kwa vitendo kuwa mwanamke akipewa nafasi anaweza kuitumikia kwa uweledi na kufanya vizuri tofauti na ilivyozoeleka.


Diwani huyo alitoa kauli hiyo wakati akihojiwa na waandishi wa habari jijini Arusha huku akisema kuwa Rais Samia amekuwa ni alama na ameonyesha kuwa wanawake wana uwezo wa kuongoza wakipewa nafasi.


“Rais Samia amekuwa ni alama kwetu sisi wanawake na ametuoyesha kuwa wanawake wana uwezo wa kuongoza wakipewa nafasi hata za juu “alisema Diwani Husna 


Alimpongeza Rais Samia kwa kumwaga fedha za ujenzi wa zahanati mbalimbali nchini ambapo katika kata ya Mbuguni ametoa jumla ya sh,50 milioni za ujenzi wa jengo la Mama na Mtoto ambao ulikwama tangu mwaka 2019.


Hatahivyo,ameishauri serikali iongeze fedha za kutosha kwa ajili ya kuwakopesha wanawake,vijana na walemavu kwa kuwa mwitikio umekuwa mkubwa sana.


Serikali hutoa fedha kwa halmashauri mbalimbali nchini kwa ajili ya kukopesha makundi mbalimbali ambapo wanawake hupewa asilimia 4,vijana asilimia 4 huku walemavu wakiambulia asilimia 2.


Diwani huyo alisema kwamba serikali inapaswa kuweka mpango mkakati wa kuongeza fedha za kutosha kwa halmashauri mbalimbali kwa kuwa fedha zinatolewa kwa sasa hazitoshi na mwitikio wa kukopa fedha hizo umekuwa ni mkubwa.


Diwani huyo alisema kwamba halmashauri nyingi nchini hazina mapato ya kutosha kwa kuwa zinategemea mapato ya fedha za ndani ambazo hazitoshi.


“Serikali inapaswa kuongeza fedha za kutosha kwa halmashauri mbalimbali nchini ili ziweze kutoa mikopo kwa makundi ya wanawake,vijana na walemavu kwa kuwa halmashauri nyingi zinategemea mapato ya ndani ambayo hayatoshi na ukizingatia mwitikio umekuwa ni mkubwa sana “alisema Diwani huyo 


Hatahivyo,alisisitiza kuwa wabunge na madiwani kupitia mikutano wanayoifanya wanapaswa kutoa elimu na mrejesho kwa wananchi kuhusu mikopo inayotolewa kwa lengo la kuongeza mwamko.


Alisisitiza kuwa ni muda mwafaka sasa serikali ina wajibu wa kutengeneza programu ya kutoa elimu ya kutosha kuhusu mikopo inayotolewa na halmashauri mbalimbali nchini kwa kuwa eneo la upande wa elimu bado ipo chini.


“Lakini pia maafisa maendeleo wa kata wawatembelee hawa wakinamama na kuzungumza nao kuhusu hii mikopo ili wapate mrejesho na kuwapa hamasa “alisisitiza Husna 


Share To:

Post A Comment: