Sheikh wa Mkoa wa Singida, Issa Nassoro, akizungumza katika usiku wa Stara, uliofanyika hivi karibuni Ukumbi wa Chuo cha Utumishi wa Umma. ambapo mada mbalimbali zinazohusu ndoa na kupinga matukio ya unyanyasaji wa kijinsia zilitolewa.

Sheikh wa Mkoa wa Singida, Issa Nassoro, akiwa na viongozi mbalimbali katika shughuli hiyo.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Yusuph Mwandami, ambaye alikuwa mgeni rasmi akizungumza kwenye usiku huo wa Stara.

Ustadhi Jafari kutoka Morogoro akitoa mada kuhusu masuala ya ndoa.

Usiku wa Stara ukiendelea.
Wanawake wakiwa kwenye usiku huo wa Stara.
Usiku wa Stara ukiendelea.
Qaswida ikipigwa kwenye usiku huo.

 

Na Dotto Mwaibale, Singida

 

BARAZA Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA), Mkoa wa Singida limeweka mkakati wa kushirikiana na Jeshi la Polisi kwa ajili ya kukomesha vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia, ulawiti na ubakaji ambavyo vimeshika kasi mkoa huu.

Sheikh wa Mkoa wa Singida, Issa Nassoro, akizungumza juzi katika usiku wa Stara, alisema maadili yamezidi kuporomoka katika mkoa huu na kuufanya kuwa wa kwanza katika matukio ya unyanyasaji wa kijinsia.

"Takwimu zinaonyesha masuala ya unyanyasaji wa kijinsia, ulawiti na biashara ya binadamu mkoa wetu umetajwa kuongoza, hili sio jambo jema inauletea sifa mbaya mkoa wetu," alisema.

Sheikh Nassoro alisema hivi sasa kumeibuka tukio la ubakaji kuanzia saa 11:00 hadi 12:00 jioni ambapo baadhi ya madereva wa bajaji wamekuwa wakibaka wanawake na watoto wanapowachukua kama abiria kwenye vyombo vyao vya usafiri.

Alisema kutokana na kukithiri kwa vitendo hivyo BAKWATA imekuwa ikishirikiana na Jeshi la Polisi katika kuhakikisha matukio hayo yanakomeshwa ambapo kuna kitengo cha kushughulikia masuala ya kijinsia katika ofisi ya sheikh wa Mkoa.

Aidha, Sheikh Nassoro alitangaza kupiga marufuku watoto kusafirishwa kwenda nje ya mkoa huu kwa ajili ya kufanya kazi za ndani kwani vitendo hivyo ndivyo vinachochea matukio ya  unyanyasaji wa kijinsia.

"Hivi sasa tumeweka utaratibu mtoto yeyote anayesafirishwa kutoka Singida kwenda mikoa mingine au nje nchi ni lazima atambulishwe kupitia ofisi ya BAKWATA mkoa ili kutunza taarifa zake ili hata akipata changamoto yoyote anasaidiwa," alisema.

Naye Mkaguzi Msaidizi wa Jeshi la Polisi anayeshughulikia Dawati la Jinsia, Damas Mwakisabwe, alisema matukio ya kulawiti, ubakaji na unyanyasaji wa kijinsia yamekuwa janga kubwa katika Mkoa wa Singida.

Mwakisabwe alisema matukio haya yanatokea kutokana na wazazi kusahau majukumu yao ya kuwalea watoto wao katika maadili na hivyo kujiingiza katika vitendo vibaya.

"Zipo kesi nyingi za matukio ya unyanyasaji wa kijinsia ambayo Jeshi la Polisi inapata na cha kushangaza matukio haya baadhi ya watoto wanafanyiwa wakati mwingine na ndugu zao wa karibu," alisema.

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Yusuph Mwandami, ambaye alikuwa mgeni rasmi alisema kumekuwa na watoto wengi wa mitaani na kwamba kuna haja kwa viongozi wa dini wakae upya na serikali kuangalia sheria ya ndoa ili ifanyiwe marekebisho.

"Hili ongezeko la watoto wa mitaani ni changamoto na linasababishwa kuwepo kwa ongezeko la wanadoa yaani  baba na  mama kuachana na hivyo watoto kukosa mlezi," alisema.

 

Share To:

dotto mwaibale

Post A Comment: