Mwandishi wetu,Arusha 

Umoja wa baraza la mawaziri wa jumuiya ya nchi za Afrika zinazozalisha almasi (ADPA) umekubaliana kusimamia biashara ya madini aina ya almasi ili kuzinufaisha nchi wanachama.

Waziri wa madini nchini,Dotto Biteko amesema kwamba mkutano wa baraza la mawaziri kwa nchi zinazozalisha almasi umekutana jijini Arusha kwa lengo la kuidhinisha nyaraka muhimu za baraza hilo,kuteua sekretarieti sanjari na kuhakikisha nchi za Afrika zinakuwa na sauti moja katika kusimamia madini ya almasi.

Waziri Biteko amesisitiza kuwa wajumbe wa baraza hilo wataupitia upya mfumo wa umoja huo na kujifunza katika eneo la usimamizi wa madini ya almasi barani Afrika ili yaweze kuwanufaisha waafrika.

amesema kuwa duniani kote madini ya almasi yana urasimu na mlolongo mpana hivyo mkutano huo utatoa fursa wajumbe kuchambua na kuangalia vigezo kwa baadhi ya nchi barani Afrika zilizopigwa marufuku kufanya biashara ya almasi duniani.

“Tutaupitia upya mfumo wa umoja wetu ikiwemo katiba na kuboresha miongozo mbalimbali katika eneo la usimamizi wa madini ya almasi Barani Afrika “alisisitiza Biteko 

Tanzania ni mwenyekiti na mwenyeji wa mkutano wa ADPA ambapo umoja huo unajumuisha nchi 18 barani Afrika ambapo nchi 12 wanachama na 6 ni waangalizi. 


Hata hivyo,Waziri Biteko amesema licha ya changamoto ya janga la UVIKO-19 Tanzania imeendelea kufanya vizuri katika mauzo ya madini aina ya almasi katika soko la dunia.

Waziri Biteko amesema kwamba baada ya janga la UVIKO-19 bei ya almasi duniani ilianguka  lakini kwa sasa almasi imepanda juu na kuifanya Tanzania kuendelea kufanya vizuri duniani.

Waziri Biteko amesema kuwa hivi karibuni kupitia mgodi wa almasi wa Mwadui uliopo mkoani Shinyanga serikal imeuza jiwe moja la almasi lenye kareti sita kwa thamani ya dola milioni 12 katika soko la dunia jambo ambalo linaashiria mafanikio makubwa kwa nchi.

“Huu uzalishaji haujawahi kutokea katika mgodi wetu wa Mwadui kwani tumeuza jiwe moja la almasi ya pink kwa thamani ya dola milioni kumi na mbili haya ni mafanikio makubwa sana kwa nchi yetu “alisema Biteko 

Waziri Biteko amesema kwamba pamoja na mgodi wa Mwadui kusimamisha uzalishaji kwa muda kutokana na ukarabati lakini kwa sasa serikali imeongeza hisa kutoka asilimia 25 mpaka 35 kama juhudi za kuongeza uzalishaji wa almasi hapa nchini.

Mwisho
Share To:

TANGA RAHA BLOG

Post A Comment: