Na Deogratius Temba- Dodoma

Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), leo Jumatatu Juni 13,2022 imewakutanisha wananchi wanaotoka katika Vituo vya Taarifa na Maarifa wilaya za Kishapu, Ubungo, Ilala na Kinondoni na wabunge wa majimbo yao Bungeni Dodoma.


Wananchi hao walifika jijini Dodoma kwa lengo la kuwasilisha changamoto zinazowakabili katika ngazi za vijiji na mitaa ambazo hazikupangiwa bajeti katika ngazi ya Halmashauri na kuziwasilisha kwa wabunge wanawake (TWPG) na wabunge wa majimbo yao ili wazifikishe kwa mawaziri wa kisekta.


Mbunge wa Kishapu, Mhe. Boniphace Butondo, amekutana na wananchi wanaotoka katika kata za Kiloleli, Mwaweja, Ukenyange, Maganzo, Songwa, Mondo, Mwaduiluhumbo, Bunambiu na Kishapu, ambapo pamoja na mambo mengine amewaahidi kuwa masuala yote atayawasilisha kwa mawaziri husika.


"Masuala haya hasa hili la Maji kwa Kiloleli, Mwaweja, Mwaduikuhumbo na Mondo, nimeshazungumza na mawaziri mara kadhaa, na tumepata fedha zaidi bil. 6 Kishapu kwenda kwenye miradi ya maji, lakni pia kwa kipindi hiki Ofisi ya Makamu wa Rais-Mazingira wametupatia zaidi ya mil. 500 kwaajili ya kuboresha mabwawa ya maji likiwepo la Kiloleli," alisema Butondo
Aidha, ameongeza kwamba bado anaendelea kushauriana na wataalamu na wadau mbalimbali ili kuvipatia vijiji vya kata ya Kiloleli maji kutokea mradi wa kata ya Ngofira ambapo ni takribani kilomita 17 kufika Kiloleli.


Wabunge wengine ambao wamekutana na kufanya mazungumzo na Vituo vya Taarifa na Maarifa ni Mbunge wa Jimbo la Ukonga Jerry Silaa na Prof. Kitila Mkumbo wa Ubungo.


Lakini pia wamepata nafasi ya kusalimiana na Waziri wa Kilimo, Husein Bashe, ambapo wananchi wa kata ya Saranga wanaotengeneza mbolea kwa kutumia taka, wamewasilisha changamoto zao na nia yao ya kutaka kuanzisha kiwanda cha mbolea inayotokana na taka.




Share To:

Post A Comment: