Na John Walter-Babati
Mwenge wa uhuru katika Halmashauri ya mji wa Babati umezindua mradi mkubwa wa maji unaotarajiwa kukamilika hivi karibuni na kuwaondolea adha wananchi kufuata maji umbali mrefu na kutumia maji ambayo sio salama.
Akiwa katika halmshauri ya mji wa Babati leo juni 16,2022, Kiongozi wa Mbio za Mwenge  wa Uhuru Kitaifa  Sahil Geraruma amekagua na  kuweka jiwe la msingi mradi wa maji  Dareda-Singu-Sigino-Bagara wenye thamani ya shilingi bilioni 12,724,407.85 fedha kutoka serikali kuu kupitia wizara ya maji.
Aidha ameipongeza mamlaka ya maji na usafi wa mazingira mjini Babati (BAWASA) kwa kusimamia vyema ujenzi wa mradi huo na kuwataka waukamilishe kwa muda uliopangwa.
Afisa biashara wa Mamlaka ya maji safi na usafi wa Mazingira mjini Babati (BAWASA) Mhandisi Rashid Chalahani amesema mradi huo una uwezo wa kuzalisha maji lita 56,000,000 kwa siku wakati wa msimu wa mvua na lita 28,000,000 wakati wa kiangazi.
Hata hivyo kwa sasa hali ya upatikanaji wa huduma ya maji katika maneo ya Dareda,Singu,Sigino na Bagara ni asilimia 38 hivyo mradi huo ambao chanzo chake ni Mto Endala ulioko kitongoji cha Bacho kijiji cha Dareda kati ukikamilika utafanya kufikia asilimia 95.
Jumla ya wananchi 80,000 wa kata hizo wanatarajia kunufaika na mradi huo wa Maji.
Kauli mbiu ya Mbio za Mwenge wa uhuru mwaka 2022 "Sensa ni msingi wa mpango na maendeleo; Shiriki kuhesabiwa,tuyafikie maendeleo ya Mwenge ya Taifa".

Share To:

Post A Comment: