Na John Walter-Babati

Kiongozi wa Mbio za Mwenge  wa Uhuru Kitaifa mwaka 2022 Ndugu Sahili Geraruma amekabidhi pikipiki 20 kwa vijana wa vikundi vitatu vya bodaboda halmashauri ya wilaya ya Babati zenye thamani ya shilingi milioni milioni 54,208,000.
Mradi huo ambao ni wa mkopo wa asilimia 4 kwa vijana kutoka kwenye mapato ya ndani ya Halmashauri unajumuisha vikundi kutoka Galapo,Mamire na Qash.
Akikabidhi pikipiki hizo Geraruma amewataka vijana hao wakazitumie katika kuinua uchumi wao na familia zao na kuepuka kuzitumia kusafirisha dawa za kulevya au kwenye uhalifu wowote.
Aidha Kiongozi huyo wa Mwenge  ameipongeza Halmashauri ya wilaya ya Babati kwa hatua hiyo akisema kuwa lengo la serikali ni kuhakikisha asilimia kumi ya mikopo kwa kila halmashauri inawafikia walengwa ambao ni vijana, Wakina mama pamoja na watu wenye ulemavu ili kuwainua kiuchumi na kuwaondoa kwenye utegemezi.
Ameongeza kuwa pikipiki hizo zikitumika kama ilivyokusudiwa zitawasaidia kupunguza wimbi la vijana kuzurura,kukaa vijiweni na kutumia dawa za kulevya ambayo yana athiri nguvukazi ya taifa.
Kwa upande mwingine amewataka vijana hao waendesha bodaboda wazingatie na kutii sheria za usalama barabarani ili kuepuka ajali zinazosababisha ulemavu wa kudumu  na hata vifo.
"Mimi siwezi nikaondoka alafu nikasikia Kuna mtu kaangia kwenye uvungu wa fuso kakatwa miguu,sitaki kusikia kitu kama hicho Sasa nataka kuacha madereva ambao wanajielewa hivyo hawa ambao bado hawajelezwa sheria za usalama barabarani warudi darasani ndo wapewe leseni na ambao leseni zao zimeisha wakachukue mpya" alisisitiza Geraruma
 Mwenge wa Uhuru leo juni 16,2022 umeingia katika halmashauri ya mji wa Babati baada ya kukikimbizwa salama katika halmashauri ya wilaya ya Babati na kutoa jumbe mbalimbali za mwaka 2022 ikiongozwa na Sensa ni msingi wa Mipango ya maendeleo,shiriki kuhesabiwa tuyafikie maendeleo endelevu ya taifa.
Share To:

Post A Comment: