Na John Walter-Kiteto

Mwenge wa Uhuru Kitaifa umeweka Jiwe la msingi kwenye mradi wa maji  Majengo mapya Kaloleni wilayani Kiteto mkoani Manyara kwa lengo la kuwezesha wananchi kuendelea kupata huduma ya maji safi. 

Mradi huo ambao uliibuliwa na wakala wa maji na usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) kwa kushirikiana na jamii na halmashauri ya wilaya ya Kiteto kutokana na changamoto ya mahitaji ya upatikanaji maji katika kata hiyo, unatekelezwa kupitia fedha za uviko 19 kwa kuchimba kisima chenye urefu wa mita 160 ambao kina uwezo wa kuzalisha maji lita 18,000 kwa saa.

Akiongea wakati wa hafla ya uwekaji wa jiwe hilo kwenye mradi huo, Kiongozi wa Mbio za Mwenge Kitaifa,Sahili Geraruma amesema ameridhika na utekelezaji wa mradi huo na kwamba utanufaisha wakazi wengi wa Kaloleni na maeneo ya jirani.

"Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan anawapenda wakazi wa Kiteto na ndio maana amewezesha mradi huu kutekelezwa kwa kasi ili kumtua mama ndoo ya maji kichwani," amesema

Ameongeza kuwa hii ni sehemu ya nia njema ya Rais Samia aliyonayo ya kuhakikisha wananchi wote wanapata majisafi ipasavyo.

Ameitaka RUWASA kuhakikisha huduma ya maji inakua endelevu na wananchi wanapata majisafi muda wote.

Taarifa kuhusu mradi huo kutoka RUWASA inaeleza kuwa mradi huo umefikia asilimia 89 ya utekelezaji na unatarajia kukamilika Juni 30 mwaka huu kwa gharama ya shilingi milioni 445,043,973.38.

"Pia mradi umehusisha uwekaji wa mtandao wa kusambaza na kulaza bomba za maji kwa kwa umbali wa mita 10,627.," imeeleza.

Mkuu wa wilaya ya Kiteto Mbaraka Al Haji Batenga ametoa shukrani kwa Serikali kwa kuona umuhimu wa mradi huo na kutoa fedha kwa ajili ya kuwezesha utekelezaji wa mradi huu kwa kasi.

Mradi wa Maji Kaloleni utakapokamilika utahudumia wananchi takribani 2,838.

Kauli mbiu ya Mwenge wa Uhuru mwaka 2022, Sensa ni msingi wa mipango ya maendeleo,shiriki kuhesabiwa,tuyafikie maendeleo ya taifa.

Share To:

Post A Comment: