Serikali imeanza kutekeleza ujenzi wa kituo mahiri cha mafunzo kwa wakulima na usimamizi wa mazao baada ya mavuno mkoani Dodoma kupitia Mradi wa Kupambana na Sumukuvu (TANIPAC) chini ya Wizara ya Kilimo mradi ambao utagharimu kiasi cha Tsh 18.3bn

Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe Anthony Mavunde ametembelea mradi wa ujenzi wa kituo hicho unaotekelezwa katika eneo la Mtanana, Wilayani Kongwa Mkoani Dodoma.

"Mhe. Samia Suluhu Hassan ametuongezea bajeti ya kilimo kutoka bilioni 294 hadi kufikia bilioni 953 mwaka 2022/2023, ambapo tumeweka mkazo kwenye utafiti wa mbegu bora, kuimarisha huduma za ugani, kujenga miundombinu ya umwagiliaji, ujenzi wa maghala na upatikanaji wa masoko ya mazao. Pamoja na kufanya yote hayo, bado tunahitaji kuimarisha mifumo yetu ya usimamizi wa mazao baada ya mavuno.

Mradi wa ujenzi wa kituo hicho wenye thamani ya shilingi bilioni 18.3 utajengwa sambamba na maghala na vihenge vya kisasa yenye uwezo wa kuhifadhi tani 19,000 pamoja na kiwanda cha kusaga, soko, eneo la kukaushia, hostel na nyumba ya watumishi kitasaidia kwa kiasi kikubwa katika mkakati wa Wizara kupunguza upotevu wa mazao baada ya mavuno kufikia tarakimu moja (_single digit_)ifikapo mwaka 2030.

Suala la upotevu wa mazao baada ya mavuno halianzii tu kipindi mazao yapo shambani, bali tangu maandalizi ya shamba na kipindi mkulima akiwa shambani, na ndo maana Kituo hicho kinajengwa ili wakulime waweze kupata mafunzo stahiki ya usimamizi wa mazao tangu yakiwa shambani mpaka baada ya mavuno.

Ninawataka wakandarasi wanaojenga mradi huo kukamilisha kwa wakati na kwa ubora ndani ya muda ambao ni Oktoba 2023, ili wananchi waanze kunufaika na matunda ya huduma zinazotegemea kutolewa kwenye kituo hicho”Alisema Mavunde

Naye Mkuu wa Wilaya ya Kongwa, Remidius Emmanuel alieleza kuwa yeye na Timu ya Wilaya wataendelea kutoa ushirikiano wa dhati kwa Wizara na wakandarasi wanaojenga mradi huo ili uweze kukamilika kwa wakati. 

Aidha, alimweleza Mavunde kuwa kuanza kutekelezwa kwa mradi huo kumeanza kuleta mafanikio kwa wananchi wa Kongwa ikiwemo kupata ajira rasmi na zisizo rasmi, kuongezeka kwa thamani ya maeneo yanayozunguka mradi na mapato kwa Halmashauri kutokana na ushuru na tozo mbalimbali.









Share To:

Post A Comment: