Na Joel Maduka, Geita. 


Kampuni ya uchimbaji dhahabu ya Geita Gold Mining Limited (GGML) imeendelea kutekeleza miradi ya elimu yenye matokeo chanya kwa wanafunzi wa kike na kiume mkoani Geita. 


Kuanzia mwaka 2018 hadi 2022, kampuni ya GGML kupitia fedha za wajibu wa kampuni kwa jamii (CSR) zilizotolewa na kampuni hiyo kwenye halmashauri ya Mji Geita, imetumia zaidi ya shilingi bilioni 13 kukabiliana na changamoto ya elimu ikiwemo uhaba wa madarasa, madawati na miundombinu mingine.


Matokeo chanya ya fedha hizo ni pamoja na ujenzi wa shule mpya ya sekondari ya Mkangala/Kanyala ambayo imetumia jumla ya shilingi za Kitanzania 150,000,000/- kutoka katika fedha zilizotolewa na Mgodi wa GGML.

Mkuu wa shule ya Mkangala Mwl. Egberth Kamugisha amesema kuwa ujenzi wa shule hiyo umekuwa msaada mkubwa kwa kuwa watoto wengi katika eneo la Mkangala walilazimika kusafiri zaidi ya kilomita sita (6) hadi shule ya Sekondari Kasamwa.


“GGML na Halmashari wametusaidia katika ujenzi wa madarasa ambayo yalitusaidia mwaka 2021 kuwahamisha wanafunzi 220 waliokuwa wakisafiri umbali mrefu kutoka eneo hili hadi Sekondari ya Kasamwa kwa ajili ya masomo. Mwaka 2022 tumepokea wanafunzi wengine 212 wa kidato cha kwanza ambao sasa wanaifanya shule yetu iwe na jumla ya wanafunzi 432,” alisema Mwalimu Kamugisha.


Kwa upande wake mwanafunzi Elizabeth Mayala anayesoma kidato cha kwanza katika shule ya Mkangala ameelezea faida za ujenzi wa shule hiyo.


“Tulikuwa tukiwaona dada na kaka zetu wakiamka alfajiri sana kwenda kupata elimu katika shule ya Sekondari ya Kasamwa. Ujenzi wa shule hii mpya umeleta nafuu kubwa. 


Ninaushukuru pia mradi wa shule hii kwa kuwa umetoa ajira kwa baba yangu mzazi ambaye amepata ajira ya muda mfupi kujenga shule hii. Hii inamsadia yeye kunilipia ada na kutupatia mahitaji muhimu ya kila siku,” ameeleza mwanafunzi Elizabeth.


Meneja mwandamizi anayeshughulikia ushirikiano wa Geita Gold Mining Limited na wadau mbalimbali, Bw Manace Ndoroma  amesema kuwa GGML ambayo inafanya shughuli zake nchini Tanzania imekuwa ikitambua thamani ya elimu kwa watoto wa kike na kiume siku zote.


“Tunapenda jamii inayozunguka migodi tunayofanyia kazi ifaidike kutokana na shughuli za uchimbaji dhahabu.


Tumekuwa tukishirikiana vizuri na serikali kulipa kodi, tozo na fedha za wajibu wa kampuni kwa jamii kwa lengo la kuhakikisha uwepo wa kampuni yetu unakuwa na tija kwa jamii inayotuzunguka,” alisema Bwana Manace.


GGML imekuwa kinara wa uwekezaji kwenye jamii tangu kuanzishwa kwake mwaka 2000 ambapo vipaumbele vikuu vimekuwa ni miradi ya elimu, afya, maji, barabara, miradi ya kukuza kipato na miradi mingine mingi ya kijamii ili kuhakikisha jamii mwenyeji inapata maisha bora. 


Mapema mwaka huu, GGML iliibuka mshindi wa jumla katika kampuni zinazofanya vizuri kwenye sekta ya madini nchini Tanzania kwa mwaka wa fedha 2020/2021 baada ya kunyakua tuzo katika vipengele vya uwajibikaji wa kampuni kwa jamii, mazingira, usalama, mlipaji bora wa mapato (kodi) na uendelezaji wazawa.


Share To:

Post A Comment: