Mkuu wa mkoa wa Arusha John Mongela akitoa cheti Cha Pongezi kwa mdau wa Maendeleo nchini na Katibu wa Kamati ya Maridhiano Sheikh Ayoub Hussein Jumaa baada ya kuleta wadau hao wa Maendeleo kutoka nchini Oman

Mkuu wa mkoa wa Arusha John Mongela akiwa na wageni wake wadau wa Maendeleo waliochimba visima katika Wilaya ya Arumeru kwenye Halmashauri ya Meru walipofika Ofisini Mapema leo
Mkuu wa Mkoa wa Arusha John Mongela akimpa tunzo ya kutambua mchango wake katika juhudi za maendeleo ya kuisaidia serikali kwa Sheikh Nasr Masoud kutoka nchini Oman Mapema leo Jijini Arusha

Na Ahmed Mahmoud 

Zaidi ya wanafunzi 2,500 katika shule tatu za Sekondari na shule mbili za Msingi za Halmashauri ya Meru, Wilayani  Arumeru  wamenufaika na huduma ya maji  baada ya kuchimbiwa visima vitano na wadau wa Maendeleo kutoka nchini Oman.


Mkuu wa Mkoa wa Arusha John Mongela amempongeza Nasr Masoud Aljahadhamy  kutoka Oman pamoja na wenzake wa kundi Sogozi la Tuelekezane Peponi kwa kuchimba visima vinne vya  maji katika Shule za  Sekondari patandi Maalum, Shule ya Sekondari Makiba,Shule ya Sekondari Kitefu ,Shule ya msingi Miembeni pamoja na kuzibua kisima kimoja  katika shule  ya msingi Patandi.


Aidha,Mongela amekabidhi zawadi  za vikombe na vyeti vya kutambua mchango wa wadau hao  kuunga mkono juhudi za Serikali katika uboreshaji wa miundombinu mbalimbali ikiwemo ya ya maji mashuleni sanjari na ahadi ya kuleta vifaa vya kusaidia shule hizo


Mkurugenzi  Mtendaji wa Halmashauri ya Meru Mwl. Zainabu Makwinya ambaye Halmashauri yake imenufaika, amesema chimbuko la kupata wadau hao ni  kupitia maadhimisho ya siku  ya  wanawake ambapo  walichanga zaidi ya  Milioni 3.6 kwa ajili ya  wanafunzi wa Shule ya Sekondari Patandi Maalum na shule ya Msingi Patandi ambapo shule hizi zinawanafunzi wenye mahitaji maalumu.


Aidha Mwl.Makwinya amewashukuru Sheikh Ayubu Hussein,Shahidu Ally na Hassan Fazal PCP  kwani siku wanawake wa Meru wakikabidhi mchango wao katika  shule ya Sekondari Patandi Maalum walikutana na  Masheik hao wakiwasilisha  sadaka ya Iftar na Daku kwa wanafunzi  ambapo waliahidi kuwakutanisha na  Ndg.Nasr Masaoud Aljahadhamy kutoka nchini Oman 


"Tunawashukuru wadau wa Maendeleo kutoka nchini Oman kwa moyo wao wa kutuchimbia visima pia wametuahidi kutuletea vifaa kadhaa kama printa vitimwendo, Mablanket n.k. hivyo kupunguza adha ya upatikanaji wa maji kwani serikali imewekeza fedha nyingi sana katika miundombinu ya shule"


Kwa Upande wake Nasr Masaoud Aljahadhamy  amesema mpaka sasa wameshachimba visima 56  hapa nchini na wataendelea kusaidia katika zoezi hilo kwa kushirikiana na serikali katika kusaidia  kusogeza mbele maendeleo


Awali, Afisa Elimu Sekondari wa Halmashauri ya Meru  Emmy Mfuru amesema kupatikana kwa huduma hiyo  ya maji ni muhimu sana haswa kwa shule za wanafunzi wenye mahitaji maalum kwani suala la usafi na mazingira hutegemea maji ambapo amefafanua upatikanaji huo wa maji  ni chachu ya  uboreshaji mazingira ya kujifunzia na kufundishia .


Nae Mdau wa Maendeleo  nchini Sheikh Ayoub Hussein  Jumaa ameishukuru  serikali kwa kuendelea kushirikiana  na wadau mbalimbali wakiwemo  viongozi wa dini katika kuwaletea wananchi maendeleo.










Share To:

Arusha Newsroom

Post A Comment: