Said Oswayo anayedaiwa kumuua kwa kumpiga risasi kadhaa mke wake Swalha Salum (28) naye amekutwa amejiua kwa kujipiga risasi.

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Mairi Makori amethibitisha kujiua kwa mtuhumiwa huyo ambaye mwili wake umekutwa ndani ya maji ya Ziwa Victoria kwenye ufukwe wa Rock Beach jijini Mwanza.

"Mwili huo umeopolewa ziwani eneo la ufukwe wa Rock Beach ukiwa na majeraha ya risasi kichwani. Timejiridhisha kuwa ndiye mtuhumiwa baada ya kutambuliwa na ndugu zake," amesema Kaimu Kamanda huyo.

Amesema mwili huo ulikutwa unaelea ufukweni mwa Ziwa Victoria ufukwe wa Rock Beach ambapo Jeshi la Polisi lililazimika kuwatafuta ndugu kwa utambulisho na kuthibitisha kuwa mtuhumiwa aliyekuwa anasakwa kwa mauaji ya mke wake.

Taarifa za uhakika zilizopatikana zinaeleza kuwa askari polisi wanaopeleleza tukio hilo walipiga kambi eneo la ufukwe wa Malaika kutokana na mawimbi ya mwisho ya mawaskliano ya mtuhumiwa Oswayo kuonekana eneo hilo kwa mara ya mwisho usiku wa kuamkia jana Mei 29.

"Mawasiliano ya mwisho ya simu ya Oswayo yalifanyika usiku wa manane eneo la Malaika; ndio maana Askari Polisi waliweka kambi pale na kweli mwili wake umepatikana hapo hapo," amesema mmoja wa watoa taarifa wetu kwa sharti la kuhifadhiwa jina

Oswayo anadaiwa kumuua mkewe kwa kumpiga risasi kadhaa katika tukio lililotokea nyumbani kwao eneo la Mbogamboga Buswelu wilayani Ilemela Mei 28 usiku.

Kabla ya mauaji hayo, wanandoa hao waliofunga pingu za maisha Desemba 31, 2021 walikuwa na ugomvi unahusishwa na wivu wa kimapenzi.

Share To:

Post A Comment: