Afisa Vijana Mkoa wa Singida, Frederick Ndahani (kulia) kwa niaba ya mkuu wa mkoa wa Singida akimkabidhi Mratibu wa Kituo cha Upendo Home for Street Children, Afesso Ogenga, msaada wa mbuzi vyakula na vitu vingine vilivyotolewa na mkuu wa mkoa huo Dk..Binilith Mahenge kwa ajili ya zawadi ya Sikukuu ya Pasaka kwa watoto  Yatima na waishio katika Mazingira magumu wanaolelewa kituoni hapo kilichopo Manispaa ya Singida katika hafla fupi iliyofanyika jana.

Afisa Vijana Mkoa wa Singida, Frederick Ndahani akiwa katika picha ya pamoja na watoto hao na Mratibu wao baada ya kukabidhi msaada huo.

 Afisa Vijana Mkoa wa Singida, Frederick Ndahani akiwa na Mlezi na Wanafunzi wa Kiislam wa Chuo cha Utumishi Singida baada ya kuwakabidhi msaada wa futari uliotolewa na Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dk.Binilith Mahenge. 


Na Dotto Mwaibale, Singida


MKUU wa Mkoa wa Singida Dkt. Binilith Mahenge amekabidhi zawadi mbalimbali  kwa kituo cha kulelea watoto Yatima na waishio katika mazingira magumu cha Upendo Home for Street Children kilichopo Manispaa ya Singida.

Zawadi zilizokabidhiwa kwa Yatima na watoto waishio katika Mazingira ni pamoja na mbuzi mmoja, mchele, mafuta ya kupikia,sukari, sabuni, unga na vitu vingine vidogo vidogo. 

Afisa Vijana Mkoa wa Singida, Frederick Ndahani akizungumza kwa niaba ya mkuu wa mkoa wakati akikabidhi msaada huo alisema mkuu wa mkoa ametoa zawadi hizo ili watoto hao wapate chakula na kufurahia sikukuu ya Pasaka kwa kuwa anaguswa na kutambua uwepo wa watoto Yatima na waishio katika Mazingira magumu waliopo mkoani hapa.

Ndahani alisema kuwa mkuu wa mkoa amesisitiza kuwa lengo la Serikali kuweka Sheria, Kanuni na miongozo mbalimbali inayosimamia vituo hivyo,uanzishwaji na uendeshwaji wake ni kuhakikisha kuwa watoto wanaolelewa katika vituo hivyo wanalelewa kwa kuzingatia utaratibu.

Aidha Ndahani alisema ni muhimu kituo hicho kuwajenga watoto katika misingi ya maadili  ya  kiroho  kusudi watoto hao wakue katika misingi ya kumjua Mwenyezi Mungu na kwamba endapo suala hilo litatiliwa mkazo Taifa litakuwa na hazina ya Raia wenye  hofu ya Mungu jambo litakalopunguza na kuondoa kabisa changamoto ya mmomonyoko wa maadili katika Taifa.

Baadhi ya watoto wanaolelewa katika kituo hicho walimshukuru Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dk. Binilith Mahenge kwa msaada huo na wakaomba msaada wa namna hiyo usiwe wa mwisho bali uwe endelevu kwani wanapopata wageni wanao watembelea wanafarijika na kujiona kama watoto wengine waliopo na familia zao.

“Tunawashukuru sana kuja kutuona na kutupatia msaada, lakini msiishie kuja kuleta misaada tu, hata kama hamna kitu msisite kuja kutusalimia na kuongea na sisi, tunaomba Mungu amzidishie mkuu wa mkoa pale alipotoa na siku nyingine tena mtukumbuke” alisema mmoja wa watoto hao.na kuahidi kumuombea kwa Mungu ili kusudi azidishiwe pale alipopunguza kusaidia watoto hao

Akizungumza baada ya kupokea msaada huo mratibu wa kituo hicho Efesso Ogenga  amemshukuru mkuu wa mkoa kwa msaadaa alioutoa kituoni hapo .

Wakati huo huo Dk.Mahenge ametoa futari kwa Wanafunzi wa Kiislam wanaosoma Chuo cha Utumishi mkoani hapa kwa ajili ya mfungo wa Mwezi Mtukufu  wa Ramadhani ambao ni moja nguzo kubwa kwa Waislamu na msaada aliotoa ni mchele, sukari, unga wa ngano na mafuta ya kula.

Akizungumza baada ya kupokea msaada huo Mlezi  wa Wanafunzi wa Kiislam chuoni hapo Abdurahaman Twahil Salama alimshukuru mkuu wa mkoa kwa msaada huo na kusema Mwenyezi Mungu atamlipa kwa kile alichokitoa na wataendelea kumuombea. 

Share To:

dottomwaibale

Post A Comment: