Mkuu wa Wilaya ya Iramba Suleiman Mwenda  (wa pili) akiwa na Wajumbe wa Kamati ya Siasa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Kamati ya Ulinzi na Usalama wa wilaya hiyo wakati wa ukaguzi wa ujenzi wa  jengo la Wagonjwa Mahututi (ICU) linalojengwa Hospitali ya Wilaya Kiomboi mkoani Singiga juzi. Kulia ni Mganga Mkuu wa Hospitali ya Wilaya Kiomboi Abel Mafuru.
Mganga Mkuu wa Hospitali ya Wilaya ya Kiomboi Abel Mafuru akitoa taarifa ya ujenzi wa jengo hilo.
Wajumbe wa kamati ya siasa ya wilaya huo wakiwa kwenye ukaguzi wa jengo hilo.


Mhandisi wa Wilaya hiyo, Profiri Modaha akitoa maelezo ya ujenzi wa jengo hilo.
Mkuu wa Wilaya ya Iramba, Suleiman Mwenda akizungumzia ujenzi huo wakati wa ukaguzi.
Wajumbe wa kamati hizo wakikagua matengenezo ya barabara ya Old Kiomboi-Kisinda na Doromoni.
Meneja wa TARURA Wilaya ya Iramba Mhandisi Evance Kibona akitoa taarifa ya ujenzi wa barabara hiyo.
Mjumbe wa kamati hiyo, Edward Makala akichangia jambo wakati wa ukaguzi wa barabara ya Kiomboi-Ruruma-Uwanza.
DC wa Iramba Suleiman Mwenda akielekeza jambo wakati wa ukaguzi wa barabara hiyo. Kulia ni Meneja wa TARURA Wilaya ya Iramba, Mhandisi Venance Kibona.
Katibu wa Mbunge wa Jimbo la Iramba Magharibi, David Madelu akichangia jambo wakati wa ukaguzi wa mradi wa upelekaji umeme Kijiji cha Tutu.
Muonekano ya vyumba vya maabara katika Shule ya Sekondari ya New Kiomboi.
Ukaguzi wa ujenzi wa Maabara Shule ya Sekondari ya New Kiomboi ukifanyika.
Mkuu wa Sekondari ya New Kiomboi Amadeus Kiduu akitoa taarifa ya ujenzi wa vyumba viwili vya maabara.
Mkuu wa Wilaya ya Iramba, Suleiman Mwenda (kulia) akizungumza na Wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya New Kiomboi wakati wa ukaguzi wa vyumba vya maabara.
Ukaguzi wa ujenzi wa Kituo cha Afya Kisiriri ukifanyika.
Kamati hiyo ikipokea maelezo ya ujenzi wa Kituo cha Afya Kisiriri kutoka kwa Mganga Mkuu wa Wilaya Iramba Hussein Sepoko (kulia)
Muonekano wa kituo cha Afya cha Kisiriri.
Ukaguzi wa Mradi wa Maji Kijiji cha Kisiriri ukifanyika.
Meneja wa Wakala wa Majisafi na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Wilaya ya Iramba Mhandisi Ezra Mwacha akitoa taarifa ya ujenzi wa mradi huo.

Ukaguzi wa ujenzi wa Kituo cha Afya Tyegelo ukifanyika .
DC Mwenda akisisitiza jambo wakati wa ukaguzi wa kituo hicho cha Afya.
Mganga Mfawidhi wa kituo hicho Beatrice Mashausi akitoa taarifa ya ujenzi wa kituo hicho.
Wananchi wakiwa kwenye mkutano wa hadhara katika Kijiji cha Kidaru Kyegelo.
Katibu Tawala wa Wilaya ya Iramba, Pius Sangoma akizungumza wakati akiwatambulisha viongozi mbalimbali waliohudhuria mkutano wa hadhara katika kijiji hicho.
Mkutano ukiendelea.
Kaimu Katibu wa CCM wa wilaya hiyo katika ziara hiyo ya ukaguzi ambaye pia ni Katibu wa Jumuiya ya Wazazi, Johari Selemani akizungumza kwenye mkutano huo wa hadhara ambapo aliwasihi wanachama wa chama hicho kujitokeza kugombea nafasi mbalimbali za uongozi kwenye uchaguzi wa ndani utakaofanyika hivi karibuni.

Mkuu wa Wilaya ya Iramba, Suleiman Mwenda akihutubia kwenye mkutano huo.


Na Dotto Mwaibale, Singida

                                      

ZAIDI ya Sh.Bilioni 2  zilizotolewa na Rais Samia Suluhu Hassan katika mwaka mmoja wa uongozi wake zimewawezesha  Wanawake wa Tarafa ya Kisisiri iliyopo Wilaya ya Iramba mkoani hapa kuwatua ndoo za maji baada ya kukamilika kwa mradi mkubwa wa maji uliotekelezwa kutokana na fedha hizo.

Kabla ya kutekelezwa kwa mdari huo wanawake hao walikuwa na adha kubwa na kutumia muda mwingi  kutembea umbali mrefu kutafuta maji ya visima vya kuchimba kienyeji huku wakiwa hawana uhakika wa kuyapata maji hayo ambayo hayakuwa salama kwa matumizi ya kunywa.

Hayo yamebainishwa na Mkuu wa Wilaya ya Iramba Suleiman Mwenda  wakati akiwahutubia  wananchi wa Tarafa ya Kisiriri  kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika Kijiji cha Didaru baada ya  kamati ya Siasa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya wilaya hiyo  kumaliza ziara ya siku moja ya kukagua miradi ya maendeleo  katika Tarafa hiyo juzi.

Mwenda alisema kamati hizo zilifanya ukaguzi wa miradi hiyo ili kuona nini kimefanyika katika mwaka mmoja wa uongozi wake Rais Samia Suluhu Hassan ambaye ametoa fedha nyingi  kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali.

Mwenda aliitaja miradi walioitembelea na kuikagua kwa sekta ya elimu kwa Shule za Msingi kuwa ni ukamilishaji wa darasa moja katika Shule ya Msingi Kiomboi Hospitali ambapo walipokea Sh.11,363,636.40, ukamilishaji wa darasa moja Shule ya Msingi Kisimba ambao pia walipokea Sh.11,353,636.36 ambao ujenzi wake umefikia hatua ya lenta ambao unatekelezwa kwa nguvu ya Wananchi.

Halikadharika Mwenda alitaja miradi mingine kuwa ukamilishaji wa darasa moja katikaShule ya Msingi Tulya kwa gharama ya 11,363,636.36, ukamilishaji wa ujenzi wadarasa moja Shule ya Msingi Doromoni kwa kiasi hicho hicho cha fedha kilichotolewa Shule ya Tulya ambapo  jumla ndogo ya miradi hiyo ikiwa ni Sh.45,454.,545.48.

Akiitaja miradi  ya Shule za Sekondari iliyotekelezwa kuwa ni ujenzi wa chumba kimoja cha darasa Shule ya Sekondari Kisiriri ambao umetumia Sh.20,000,000, ukamilishaji wa vyumba viwili vya maabara katika Shule ya Sekondari ya Kisana ambapo walipokea Sh.30,000,000 na ukamilishaji wa vyumba vingine viwili vya maabara katika Shule ya Sekodari ya New Kiomboi kwa gharama hiyohiyo na kuifanyajumla ndogo kuwa ni Sh.60 Milioni.

Akielezea Sekta ya Afya alisema wamejenga Kituo cha Afya Kisiriri kwa gharama ya Sh.250,000,000 na kuwa ujenzi wake upo katika hatua ya umaliziaji jengo la OPD likiwa kwenye hatua za upakaji wa rangi, kuwekwa milango na madirisha na halikadharika jengo la maabara.

Alitaja mradi mwingine wa sekta ya Afya kuwa ni ujenzi wa Kituo cha Afya Tyegelo ambao pia walipokea Sh.250,000,000, ujenzi wa choo Zahanati ya Doromoni ambao unatekelezwa kwa gharama ya Sh.40,000,000, ujenzi wa choo Zahanati ya Kisana kwa gharama ya Sh.39,950,000 jumla ndogo yake ya ujenzi wa vyoo hivyo ikiwa ni Sh.79,950,000 huku ujenzi wa Zahanati ya Tutu ukigharimu Sh. 50,000,000.

Mwenda aliongeza kuwa katika Sekta hiyo ya Afya wanakamilisha ujenzi wa wodi ya dharura (EMD) katika Hospitali ya Wilaya ambapo wamepokea Sh.300,000,000, ujenzi wa Chumba cha Wagonjwa Mahututi (ICU) kwa gharama ya Sh.250,000,000 huku jumla yake ndogo ikiwa ni Sh.550,000,000.

Aidha Mwenda akizungumzia Sekta ya barabara alisema wanafanya matengenezo ya barabara ya Kisiriri-Kisimba kilometa 9.42, Old Kiomboi-Meli-Walla-Ntwike kilometa 0.9, matengenezo ya kawaida barabara ya Kitusha-Kisana Kilometa 6.0  na ujenzi wa mifereji mita 100 kwa gharama ya Sh.126,383,800.

Alitaja mradi mwingine kuwa ni matengenezo muda maalum barabara ya Kiomboi-Ruruma-Uwanza kilometa17.4 kwa gharama ya Sh.492,019,500, matengenezo muda maalum barabara ya Old Kiomboi-Kisimba-Doromoni Kilometa 9 na kufungua barabara ya Kibigiri Masagi-Kinkungu na kufungua barabara ya Migilango kilometa 5 na na Barabara ya Mwamapuli- Luono ambazo zote kwa pamoja  jumla yake kuu ni Sh. 1,295,947,201.

Alisema mradi mwingine walioukagua ni  upelekaji wa umeme kwenye kitongoji cha Tutu ambao unatekelezwa na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kwa gharama ya Sh.122,331,420.54 ambao umekamilika kwa asilimia 100.

Akizungumza kwa nyakati tofauti  katika ziara hiyo Mwenda alisema miradi hiyo inafanyika ikiwa ni utekelezaji wa ilani ya Chama Cha Mapinduzi  (CCM) na Serikali inawajibu wa kuikagua ili kuona kama inatekelezwa kwa viwango vinavyo hitajika.

                Mwenda  alitumia nafasi hiyo kumshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha hizo na kuwaomba viongozi ilipo miradi hiyo kuwahamasisha wananchi wao kuitunza. 

.Aidha Mwenda aliwaomba wananchi kutoa ushirikiano kwa vijana wanaoshiriki katika zoezi la anuani za makazi na postikodi linaloendelea nchi nzima kwa kuwaelekeza majina ya mitaa na mambo mengine yanayohitajika na akawaomba kufanya hivyo pia katika zoezi la Sensa ya watu na makazi.

Ziara hiyo ambayo imeleta ari na mwamko mkubwa kwa wananchi wa wilaya hiyo kushiriki shughuli za maendeleo baada ya kupokea taarifa ya miradi iliyotekelezwa katika kipindi cha mwaka mmoja wa uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan ambapo pia walitumia nafasi hiyo  kumpongeza pamoja na mbunge wao Dk.Mwigulu Nchemba kwa kutoa fedha nyingi ilifanyika katika Tarafa za Ndago, Kinampanda, Shelui  na Kisiriri zenye jumla ya kata 20 na vijiji 70.

 

Share To:

dotto mwaibale

Post A Comment: