Na Mosses Mashala 

Mfanyabiashara Maarufu wa Madini ya Tanzanite Jijini Arusha,Pendael Mollel {47} Mkazi wa Kiranyi Jijini Arusha amepandishwa kizimbani na kusomewa shitaka la Mauaji.

Mbali ya Mollel wengine aliounganishwa kwenye kesi hiyo  ni pamoja na Onesmo Laizer {35} mkazi wa Ngaramtoni wilayani Arumeru ambaye pia ni mlinzi wa Mfanyabiashara huyo na mtuhumiwa mwingine Deogratias Mollel {25} mkazi wa Sakina Jijini Arusha ambaye ni Mdogo wa Mfanyabiashara huyo.

Akisoma shitaka la Mauaji, Mwendesha Mashitaka wa Serikali, Grace Medikenya  mbele ya Hakimu Mwandamizi wa Mahakama ya Wilaya ya Arusha, Devotha Msofe ilidaiwa kuwa mtuhumiwa Mollel na wenzake wawili walimuua kwa kukusudia Stephen Kivuyo {43} katika tukio lililotokea aprill 18 mwaka huu katika eneo la Burka Jijini Arusha majira ya saa 1.45 usiku.

Baada ya kusomewa shtaka hilo Hakimu Msofe aliwaeleza watuhumiwa kuwa mahakama hiyo haina Mamlaka kisheria kusikiliza kesi hiyo kwani kesi hiyo ya Mauaji itasikilizwa na Mahakama Kuu hivyo hawatakiwi kujibu chochote na kesi yao ilihairishwa hadi Mei 10 mwaka huu itakapokuja kutajwa tena.

Mollel alifikishwa mahakamani hapo chini ya ulinzi mkali wa polisi na akiwa mahakamani hapo alionekana kuwa mpole na mnyonge huku idadi ndogo ya ndugu na jamaa zake wakijitokeza mahakamani.

Marehemu Steven alizikwa nyumbani kwake Ilkiushin ,wilayani Arumeru, mkoani hapa April 26 mwaka huu, jumanne wiki hii na ameacha mjane mwenye ujauzito na wanae watano wadogo.

Share To:

Post A Comment: