Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Innocent Bashungwa amemsimamisha kazi Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero Mkoani Morogoro, Hassani Njama Hassani kuanzia leo Jumatano Aprili 20, 2022 ili kupisha uchunguzi.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Aprili 20, 2022 na wizara hiyo imeeleza kuwa Bashungwa amechukua hatua hiyo baada ya Mkurugenzi huyo kushindwa kutekeleza maagizo aliyoyatoa wakati wa ziara yake ya kikazi aliyoifanya katika Halmashauri hiyo Machi 10, 2022.

Taarifa imeeleza kuwa katika ziara hiyo waziri alibaini upotevu wa fedha za miradi na matumizi yasiyo sahihi ya Sh231.84 milioni katika ujenzi wa shule ya Sekondari ya Kumbukumbu ya Moringe Sokoine zilizotolewa kwa ajili ya ujenzi wa bwalo la chakula, jiko na bweni.

Baada ya kubaini upotevu huo waziri huyo alimuagiza Mkurugenzi kuwachukulia hatua za kiutumishi wakuu wote wa Idara na watumishi waliohusika na ukiukwaji wa taratibu za manunuzi katika mradi huo.

“ Hadi kufikia leo hii hakuna mkuu wa idala yeyote ama mtumishi aliyechukuliwa hatua kufuatia agizo hilo” imesema taarifa hiyo.

Aidha Waziri Bashungwa amewataka wakurugenzi wa halmashauri zote nchini kuendelea kusimamia miradi ya maendeleo kikamilifu.

Share To:

Post A Comment: