Na John Walter-Manyara

Watanzania leo wanaadhimisha miaka 58 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, ulioasisiwa Aprili 26 mwaka 1964.

Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ni muungano wa mataifa mawili huru ya Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar,  ambayo yaliingia mkataba wa muungano mwaka huo wa 1964 na kuanzishwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mkataba wa Muungano ulitiwa saini na aliyekuwa Rais wa Tanganyika Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na aliyekuwa Rais wa Zanzibar Hayati Sheikh Abeid Amani Karume Aprili 22 mwaka  1964 huko Zanzibar na baadaye mkataba huo ulithibitishwa na Bunge la Tanganyika na Baraza la Mapinduzi.

Katika mkoa wa Manyara, Mkuu wa mkoa huo Charles Makongoro Nyerere ameongoza viongozi na wananchi mbalimbali mjini Babati kusheherekea kumbukumbu ya Miaka 58 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar  kwa kufanya usafi na kupanda miti katika eneo la ofisi ya Halmashauri ya mji wa Babati.


Akizungumza baada ya kufanya usafi katika eneo la soko kuu la Babati,Mkuu wa mkoa wa Manyara Charles Makongoro Nyerere amewataka wananchi kutoa ushirikiano katika zoezi la Sensa ya watu na makazi iliyopangwa kufanyika Mwezi Agosti mwaka huu,kushiriki kikamilifu katika zoezi la kuweka anuani za makazi na kwenye zoezi la chanjo ya polio kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano litakaloanza April 28 hadi Mei Mosi mwaka huu.

Share To:

Post A Comment: