Na Ahmed Mahmoud

 MAHARAGWE ni moja ya chakula maarufu hapa nchini Tanzania ambacho kimewasaidia watoto wengi kukuwa wakiwa na afya njema na wenye mazingira mazuri kimaisha.

Ulaji huu wa Maharagwe umekuwa ukiangaliwa zaidi kwa watoto ambao wamekuwa wakiyapenda zaidi katika ulaji wao hasa ukichnganywa na Wali, Ugali, Mikate na hata Maandazi jambo ambalo huwafanya kufurahia chakula hicho.

Leo hii, chakula hicho kimekuwa maarufu hasa katika skuli za Dahalia, Kambi za askari, ambapo kila mlo wao ni la lazima Maharagwe yawemo ambayo ndani ya wiki huwa ni lazima yatumike kwa mara mbili ama tatu.


Chakula hichi hivi sasa kimekuwa kikizalishwa kwa aina za Mbalimbali  za maharagwe kwani yapo yanayoitwa ya Mbeya, Maharagwe ya Soya, Maharagwe Mekundu na Yakijani kibichi, ikiwa humpa mtu nafasi ya kuchagua aina aitakayo kwa kuangalia ladha anayoipenda.


Mara nyingi Maharagwe yanaonekana kama ni cha kula cha watu wa chini kisichokuwa na manufaa na kinaondolewa katika orodha ya vyakula vyenye hadhi na kisichokuwa na manufaa kwa afya. Hata hivyo ni kutokana na kwamba watu wengi wanaona vyakula kama nyama na samaki kuwa ni vya kitajiri na Maharagwe huchukuliwa ni chakula cha kimaskini, ingawa huo ni upotoshaji kwani yanafaida nyingi mwili ambazo watu wasikula wanazikosa.

Wataalamu wanasema kwamba Maharagwe ni moja ya chakula kinachoponguza lehemu mwilini, huzuia saratani, huberesha afya ya ubongo, hutawala kiwango cha sukari mwilini, huongeza nguvu za mwili na huimarisha mifupa.


Kazi nyengine ambazo Maharagwe mwilini huimarisha ngozi, huimarisha afya ya moyo, afya ya Macho, huboresha uwezo wa kumbukumbu,huondoa sumu mwilini na hukabili shinikizo la damu,.


Vile vile, Chakula hiki cha Maharagwe hupunguza uzito, husaidia tatizo la kutopata choo, husafisha tumbo, husaidia kukabili maradhi ya asthma, huboresha na kukomaza seli nyekundu, huzuia kuzeeka mapema na huimarisha afya ya kucha na nywele.Leo hii, tatizo la utapiamlo hapa nchini kwa watoto waliochini ya miaka mitano na wanawake walio kwenye umri wa kuzaa limepatiwa ufumbuzi baada ya  taasisi ya TARI Selian kuzalisha mbegu aina mbili za Maharage selian 14 na 15 maarufu kama Maharagwe Jesca.


Hiyo ni kutokana na kuona umuhimu wa kufanya utafiti huo ambao umesaidia kupata mbegu mpya ambayo imeonesha kuleta matokeo chanya kwa afya ya binadamu kwani uchunguzi uliofanywa umebainisha zina mchango mkubwa katika kuimarisha afya ya Mtoto na watu wazima.

 

Mtafiti kutoka kituo cha Utafiti TARI Selian, Shida Nestory Mahenge,akiongea kwa wanahabari wakati wa ziara ya mafunzo ya Utafiti Sayansi na Ubunifu yalioandaliwa na Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), amesema, waliamua kufanya utafiti huo ili kupata suluhu ya maradhi yaliokuwa yanawakumba zaidi watoto hasa ya utapiamlo.

 

 "Tanzania ilikuwa inakabiliwa na upungufu wa damu kwa watoto waliochini ya umri wa miaka mitano na wanawake walio na umri wa uzazi pia wanakabiliwa na upungufu wa damu, Jambo hili lilitufanya kama watafiti tuje na majawabu haya ya mbegu mbili bora za Maharage ya kuongeza Madini ya Zinki na Madini chuma"


 

Mtafiti Mahenge, anaeleza kituo hicho kimekuja na mbegu hizo za Maharage Jesca baada ya takwimu za Afya na viashiria vya malaria iliyofanyika Mwaka 2015/2016 ilionyesha kuwepo kwa upungufu wa damu kwa watoto wenye umri kati ya miezi 6 hadi 56 sawa na asilimia 58.

 

Anabainisha kwamba asilimia 26 kati yao wana upungufu wa damu wa kawaida asilimia 30 wanaupungufu wa kati huku  asilimia 2 wanaupungufu wa juu kwenye baadhi ya mikoa kama Shinyanga.

 

Kwa mujibu wa Mtafiti Mahenge anaeleza hali ni mbaya zaidi ambapo asilimia 71 ya watoto chini ya miaka mitano Wana upungufu wa damu wakati asilimia 45 ya wanawake wa Tanzania waliokatika umri wa uzazi (miaka15-49) wanaupungufu wa damu.

 


Anaeleza kwamba kiwango cha upungufu wa damu kwa Unguja ni asilimia 60, na kwa mkoa wa kaskazini Pemba ni asilimia 72, ambapo asilimia 70 ya vifo vinavyosababishwa na upungufu wa damu hutokea Afrika 

 Aina hizi mpya alisema zitaweza kukidhi mahitaji ya wakulima wadogo na wasindikaji katika kupunguza tatizo la upungufu wa damu kwa makundi yenye uhitaji mkubwa wa damu, ikiwemo maharage haya ya Jesca ambayo yanaweza kusagwa na kupikwa uji.  

Analeeza kwamba ili Kuhakikisha upatikanaji wa mbegu vituo vya Utafiti wa kilimo ikiwemo vinashirikiana na makampuni ya uzalishaji mbegu kwa wakulima na vikundi vya wakulima kwa ajili ya uzalishaji mbegu kwa wingi. Mahenge Anaeleza kwamba baada ya kujua changamoto hiyo ya upungufu wa damu kutokana na takwimu hizo na tatizo kubwa la kiafya na kilishe, jamii inahitaji ufumbuzi wa haraka wa lishe ndipo wakaja na aina ya maharage Jesca ambayo yana ubora mkubwa wa kuongeza lishe mwilini.

 

"Maharage yenye Madini hayo ya chuma na Zinki yalizalishwa hapa kituoni Selian  katika hali ya kawaida ya kiagronomia kwa aina mbili za selian 14 na selian 15" alibainisha

 

Kwa mujibu wa Mahenge Madini ya chuma na Zinki ni muhimu katika mwili wa binadamu ambapo Madini ya chuma yanaongeza chembechembe nyekundu za damu ambazo ni muhimu kwenye kusafirisha hewa ya oksijeni kwa ajili ya uhai.

 

Anabainisha kwamba Maharage haya yanafaa kupandwa ukanda ulio kati ya mita 1000-2000 kutoka usawa wa bahari hivyo yanastawi vizuri katika katika mikoa ya Mbeya Iringa Arusha Kilimanjaro Manyara Kigoma na Tanga hususani Lushoto.

 


Aliongeza aina hizi mpya zitaweza kukidhi mahitaji ya wakulima wadogo na wasindikaji katika kupunguza tatizo la upungufu wa damu kwa makundi yenye uhitaji mkubwa wa damu kwa watoto waliochini ya miaka mitano na mama wajawazito.

 

Anasema kwamba sifa ya Selian 14  yanatambaa kwenye miti yakiwa na ukubwa wa punje pia kuwa na kiwango cha Madini ya chuma 75.17-85.65 ppm ambapo kiwango cha Madini ya Zinki 26.38-41.65ppm.

 

Abainisha kuwa mavuno yake ni zaidi ya kilogramu  2000 kwa hekta na hukomaa kwa siku 90 hadi 110 ambapo yanafaa ukanda wa kati mpaka ukanda wa juu pia yanakidhana na ugonjwa wa chule na haya leti gesi tumboni.

 

Alisema kwa maharage hayo yana ladha tamu Sana  unaweza kuyapika katika mchanganyiko wowote bila kupoteza ladha yake na yana mchuzi mzito yakipikwa ambapo yanakubalika kwa wauzaji wa aina zote mashuleni hotelini nk.

 

Anabainisha sifa za selian 15 kwamba yanatambaa kwenye miti ukubwa wa punje una mbegu kubwa na kiwango cha Madini ya chuma 74.22 -81.35ppm huku Madini ya Zinki yakiwa 27.38-42.55ppm.

 

Anaeleza kwamba maharage hayo mavuno yake zaidi ya kg.2000 kwa hekta na hukomaa ndani ya siku 90 hadi 110 na yanafaa kulimwa ukanda wa kati mpaka ukanda wa juu.

 

"Zipo aina nyingine zaidi ya sita ambazo tumezifanyia utafiti hapa kituoni kwetu na zimeleta matokeo chanya kwa wakulima wetu na kuongeza tija ya uzalishaji" anaongeza Mahenge

 


Anabainisha kuwa yapo maharage aina Uyole 17 ambayo inastawi katika ukanda wa kati na wa juu kati ya mita 800-2000 kutoka  usawa wa bahari yanakomaa kwa muda wa siku 84 mavuno yake ni gunia 6 kwa ekari moja na yana ladha tamu na rangi ya kuvutia.

 

"Maharage haya hayana gesi ni mafupi yenye punje kubwa nyeupe na baka jeusi katikati Pia tuna aina ya  Uyole 18 inastawi ukanda wa kati na ukanda wa juu mita 800 kutoka usawa wa bahari inakomaa kwa muda wa siku 82 inatoa mavuno magunia 8 kwa ekari na ina ukinzani dhidi ya magonjwa mnyauko na paka pembe"anabainisha

 

Imeelezwa kwamba Maharage Jesca ambayo ni kati ya aina hizo mbili za Maharage yenye Madini ya Zinki na chuma huboresha tendo la ndoa majumbani na kujenga na kuongeza lishe.

Kutokana na utafiti huo ni wazi kuwa jamii itaweza kufaidika kupata suluhu ya tatizo ililokuwa linaikabili kwani kituo cha taasisi ya TARI Selian, kimeonyesha njia kwa kutoa mbegu mpya  ambayo ni mkombozi kwa maisha ya watoto na watu wazima.

Share To:

Arusha Newsroom

Post A Comment: