Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega(katikati) akipata maelezo kutoka kwa Meneja Msaidizi wa Mradi kutoka Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), Abdallah Fedes (kulia) kuhusu ramani ya eneo lililotengwa kwa ajili ya wafugaji kutoka katika hifadhi ya  Ngorongoro wakati wa ziara yake ya kukagua eneo hilo lililopo katika Kijiji  cha Msomera, Wilayani Handeni, Mkoani Tanga Aprili 11, 2022.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega(watatu kutoka kushoto) akikagua moja ya eneo ambalo litatumika kujenga bwawa la kunyweshea mifugo alipofanya ziara katika Kijiji  cha Msomera, Wilayani Handeni, Mkoani Tanga Aprili 11, 2022. Katika kijiji hicho kumetengwa eneo  kwa ajili ya wafugaji kutoka Wilayani Ngorongoro kuhamia hapo kwa hiari yao ili kuendeleza shughuli zao za ufugaji.

Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Mhe. Siriel Mchembe(kulia) akifafanua jambo kwa  Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega(kushoto) walipokutana katika ofisi ya Mkuu huyo wa Wilaya Aprili 11, 2022.


Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega amesema kuwa Serikali imeweka mipango mizuri ya kuhakikisha kijiji cha Msomera kilichopo Wilayani Handeni, Mkoani Tanga kinakuwa na miundombinu ya kisasa ya kuhudumia mifugo ikiwemo Majosho, Malambo na Nyanda za malisho ili wafugaji kutoka hifadhi ya Ngorongoro watakaohamia katika eneo hilo waweze kufuga kisasa na kwa tija.

Ulega aliyasema hayo Aprili 11, 2022 alipofanya ziara katika Kijiji hicho cha Msomera ambapo kuna eneo limetengwa maalum kwa ajili ya wafugaji kutoka katika eneo la hifadhi ya Ngorongoro kuhamia hapo kwa hiari yao ili kuendeleza shughuli zao za ufugaji.

Baada ya kukagua maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya Malisho, Majosho na Malambo, Mhe. Ulega alitoa maelekezo kwa Wataalam wanaosimamia uendelezaji wa maeneo hayo kuweka mikakati mizuri ya kukamilisha ujenzi wa miundombinu hiyo ili wafugaji hao kutoka ngorongoro watakapohamia eneo hilo wakute miundombinu ipo tayari na waweze kuendelea na shughuli zao.

“Tunataka wafugaji watakaokuja kufanya shughuli zao katika kijiji hiki cha msomera, wafanye shughuli zao za ufugaji kisasa, wafanye ufugaji wa kibiashara na tunataka hapa pawe ni shamba darasa ili hata mtu akitaka kujifunza ufugaji wa kisasa aletwe hapa”,alisema

Aliongeza kwa kusema kuwa Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ametoa pesa kwa ajili ya kujengwa Majosho kumi (10) Wilayani humo ili mifugo iweze kuhudumiwa vizuri huku akisisitiza kuwa ufugaji huo wa kisasa utakaofanywa kijijini hapo utasaidia viwanda hapa nchini kupata malighafi bora na za uhakika.

Mhe. Ulega aliwataka watendaji hao wanaosimamia uendelezaji wa maeneo hayo kuwa na mkakati wa pamoja ambao utaonesha utendaji wa shughuli zao kwa kila wiki na wawe wanaanda taarifa na kuzipeleka katika mamlaka husika.

Aidha, alitumia nafasi hiyo pia kuwahimiza wafugaji watakaohamia Wilayani hapo kuwa tayari kubadilika na kufanya ufugaji wa kisasa na kuachana na ufgaji wa mazoea ambao wamerithi kutoka kwa wazee wao kwani kwa sasa tija yake ni ndogo.

Naye, Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Mhe. Siriel Mchembe alisema kuwa ujio wa Naibu Waziri Ulega Wilayani humo ni faraja kwao na anaamini utasaidia kutoa msukumo kwa Wataalam kuongeza nguvu katika utendaji hususan katika sekta ya mifugo.

Aliongeza kwa kusema kwa sasa kipato cha mwananchi wa kawaida wilayani humo ni kiasi cha shilingi laki nane na kumi kwa mwaka (810,000) lakini wamejiwekea malengo kuwa ifikapo mwaka 2025 kipato hicho kiongezeke kufikia shilingi Milioni moja (1000,000) kwa mwaka na hiyo itafanikiwa kupitia shughuli za ufugaji wa kisasa unaotegemewa kufanyika katika kijiji cha Msomera.
Share To:

Post A Comment: