Naibu Waziri wa Kilimo Anthony Mavunde amewataka watafiti kuongeza kasi ya kutoa elimu kwa wakulima juu ya mbinu sahihi za kudhibiti visumbufu kwenye zao la pamba pamoja na kuhakikisha wanalifanyia kazi suala la wadudu visumbufu waliovamia zao la pamba ambao wanaweza kupelekea kushuka kwa uzalishaji wa pamba kama hatua madhubuti hazitachukuliwa mapema.


Mh.Mavunde ameyasema hayo leo tarehe 18 Machi, 2022 Wilayani Misungwi, Mwanza alipotembelea Kituo cha Utafiti wa Kilimo cha TARI Ukiriguru.


"Mmenionesha hapa namna mnavyofanya tafiti za kupambana na visumbufu kwenye zao la pamba, lakini dawa hizo hizo mlizotumia ndizo zinazolalamikiwa  na wakulima kuwa hazifanyi kazi wanapozitumia kwenye mashamba yao, hivyo wekeni mkakati wa kutoa elimu kwa wakulima juu ya taratibu sahihi za unyunyiziaji wa viuatilifu kwenye mashamba yao pamoja na kufanya uchunguzi kwa kushirikiana na Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu(TPHPA) juu ya aina ya viuatilifu vinavyotumika na ubora wake katika kutatua changamoto hii ya athari kwa pamba ya wakulima.


Suala la tija kwa mkulima si la mbegu bora na kanuni za kilimo bora pekee, tusipodhibiti visumbufu tutakuwa hatuwasaidii wakulima kuweza kufikia tija kubwa ya uzalishaji na kuongeza kipato kutokana na pamba wanayozalisha.


Lazima watafiti kuwa wabunifu na kuhakikisha tafiti zao zinajikita kutatua changamoto zinazowakabili wakulima. Serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan inawathamini watafiti na ndio maana Wizara ya Kilimo imepanga programu ya kuwajengea uwezo watafiti kwenye vyuo bora duniani kote ili waweze kuwa na ufanisi wa kugundua na kuendeleza teknolojia za kusaidia wakulima wetu nchini.


Naye Kaimu Mkurugenzi wa Kituo cha TARI Ukiriguru, **Dkt. Heneriko Kulembeka **alieleza kuwa Kituo chake kwa kushirikiana na wadau wengine kama Bodi ya Pamba, Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viautilifu (*TPHPA*) na Mamlaka za Serikali za Mikoa na Wilaya wanapanga kuanza programu za kutoa elimu ya unyunyiziaji wa viuadudu kwa maafisa ugani na vijana ambao watasaidia kuwafikia wakulima wengi zaidi wa pamba nchini ili kuongeza kasi ya udhibiti wa visumbufu vya zao la pamba.

Share To:

Post A Comment: