Na Ahmed Mahmoud Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii imekagua mradi wa TANAPA wa ujenzi wa mahema matatu ya kudumu unaogharimu kiasi cha shilingi milioni 163 katika Hifadhi ya Kisiwa cha Saanane jijini Mwanza. Akizungumza katika ziara hiyo, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii, Mhe. Ally Juma Makoa (Mb) amemuelekeza mkandarasi kuharakisha ujenzi wa mahema hayo ili kuvutia zaidi watalii wanaotembelea kisiwa hicho. “Endapo mahema haya yatakamilika na mkiongeza ubunifu wa kukitangaza kisiwa hiki kwa kutumia watu maarufu, lengo la kuongeza mapato yatokanayo na utalii litatimia”amesema Mhe. Makoa. Aidha, amewataka watendaji wa hifadhi hiyo kupima uwekezaji wa mahema hayo kama utarudisha fedha zilizotolewa na Serikali.“Ni muhimu kuzingatia ni kwa muda gani uwekezaji huu wa mahema utarudisha fedha za Serikali” amesisitiza Mhe. Makoa. Pia, ameishukuru Serikali kwa kuwekeza fedha nyingi katika Sekta ya Utalii kwa kuwa ni chanzo kikubwa cha mapato na kufafanua kuwa baada ya Royal Tour ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan mabadiliko katika kuongezeka kwa mapato yatokanayo na utalii yameonekana. Ameishukuru pia Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kuendelea kuutangaza utalii kupitia njia mbalimbali ikiwamo mikutano ya kimataifa na kuitaka Wizara hiyo kuendelea na juhudi hizo ili iweze kuongeza tija kwa nchi. Naye, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja (Mb) ameishukuru kamati hiyo kwa kutembelea Hifadhi ya Kisiwa cha Saanane na kuahidi kuendelea kutoa ushirikiano katika kuhakikisha malengo ya kuongeza idadi ya watalii yanafikiwa na mapato yatokanayo na Sekta ya Utalii yanafikiwa.
Share To:

Arusha Newsroom

Post A Comment: