Na. Asila Twaha, Shinyanga DC


Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Hesabu za Serikali za Mitaa Mhe. Selemani Zedi ameishauri  Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kutatua changamoto  za upungufu wa watumishi katika Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya  Shinyanga ili ianze kutoa huduma kwa wananchi. 


Mhe. Zedi amesema hayo wakati wa Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Hesabu za Serikali za Mitaa ilipokagua hospitali hiyo Machi, 19 2022 ikiwa ni ratiba ya muendelezo wa ziara ya kamati hiyo, mara baada ya kukagua na kuridhishwa na ukamilikaji wa hospitali kufikia hatua ya 100%. 


Ameeleza kuwa ujenzi wa hospitali hiyo umezingatia ukamilishaji wa majengo 7 ikiwemo jengo la wangonjwa wa nje, stoo ya dawa, jengo la maabara, jengo la kuhifadhia maiti, jengo la vipimo vya mionzi, jengo la kufulia nguo, jengo la wazazi na upasuaji.


Mhe. Zedi amesema, pamoja na majengo kukamilika lakini kamati imeona zipo changamoto ambazo zinaweza kusababisha kukosekana kwa huduma  mapema katika hospitali hiyo na wananchi kuendelea kufuata huduma mbali ikiwemo baadhi watumishi kustaafu na wengine kutolewa kutokana na zoezi la uhakiki wa vyeti uliofanywa na Serikali.


“Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Hesabu za Serikali za Mitaa imeishauri Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa iendelee kuchukua hatua za haraka ili kuongeza watumishi katika hospitali hiyo ili wananchi waweze kupata huduma kwa haraka” amesema Mhe. Zedi


Naye Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Dkt. Festo Dugange amesema Serikali inachukua  ushauri wa Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Hesabu za Serikali za Mitaa na kuhakikishia wanaenda kushirikiana kwa  pamoja na  viongozi katika kutatua changamoto zilizopo.


“Niwaelekeze viongozi wote wa sekta ya Afya katika Mamlaka za Serikali za Mitaa kuendelea kufanya kazi kwa uadilifu ili kuwatumikia wananchi kwa yale ambayo tunayoona tunaweza kufanya kwa kufuata maelekezo na sheria tuyafanyie kazi ili tuepuke mapungufu ambayo Halmashauri yanaweza kuyatatua  ili wananchi waweze kupata huduma” amesema Dkt. Dugange


Mhe. Zedi ameupongeza uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga  kwa kuongeza kujenga jengo la kuhifadhia maiti na jengo la kuhifadhia chanjo ambapo hapo awali hayakuwemo katika bajeti waliopewa ila kwa ubunifu wa uongozi waliweza kuongeza majengo hayo ambapo yatatumika katika kutoa huduma.


Aidha, amezishauri Halmashauri zote nchini zilizopelekewa  fedha za miradi ya maendeleo zitumike kuendana na thamani ya vitu lakini pia wajue miradi hiyo ni kwa ajili ya  wananchi kupata huduma.

Share To:

Post A Comment: