Na. Nuru Mwasampeta

 

Imeelezwa kuwa janga la ugonjwa wa Uviko-19 lililoikumba dunia mwishoni mwa mwaka 2019 limesababisha athari nyingi kwa uchumi wa nchi mbalimbali duniani ambapo athari hizo  zimejithihirisha katika Sekta ya mbolea ambapo bei ya mbolea kwenye soko la dunia imepanda na kusababisha changamoto ya bei kwa wakulima nchini.

 

Katika kuhakikisha tatizo la upatikanaji na bei ya mbolea nchini lina thibitiwa, serikali kupitia Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) imeendelea kuhamasisha wawekezaji kuwekeza katika viwanda vya mbolea na kwa viwanda vilivyopo ambavyo uzalishaji wake ni mdogo hususani vinavyozalisha mbolea ya maji (foliar fertilizers) vimeendelea kuboreshwa kwa kupanua maeneo ya uzalishaji, kufunga mashine na miundombinu mingine katika viwanda hivyo ili kukidhi mahitaji ya wakulima.

 

Hayo yalibainishwa hivi karibuni na Kaimu Mkurugenzi wa Uzalishaji wa Ndani na Ununuzi wa Mbolea kwa Pamoja, Joseph Charos alipokuwa akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa majukumu  kwenye kikao cha Bodi ya wakurugenzi wa TFRA kwa kipindi cha nusu mwaka kuanzia mwezi Julai mpaka Desemba 2021.

 

Aidha, Charos alibainisha kuwa maendeleo ya viwanda vya mbolea kwa ujumla ni mzuri kwani viwanda vilivyopo vimeendelea na uzalishaji ambapo kwa kipindi cha robo ya pili ya Mwaka wa Fedha 2021/2022 TFRA imekuwa na jukumu la kuhamasisha matumizi ya mbolea zinazozalishwa ndani ya nchi kwa wakulima.

 

Pamoja na hayo, Charos alibainisha kuwa, maendeleo ya wawekezaji wapya walioonesha nia ya kuwekeza na walioanza ujenzi wa viwanda vya mbolea nchini   wanaendelea vizuri. Anasema  ujenzi wa kiwanda cha Mabwepande Composite Manure umekamilka na uzalishaji wa  mbolea kwa ajili ya majaribio unaendelea .

 

Aliongeza kuwa, ujenzi wa kiwanda kipya cha mbolea cha Itracom kinachojengwa Jijini Dodoma na mwekezaji fertilizer limited kipo katika hatua mbalimbali za ujenzi  ikiwemo uzio, majengo ya ofisi, maghala na majengo ya kiwanda, ujenzi huo umefikia asilimia 57%, aidha  mitambo ya kuzalishia mbolea iliyowasili katika eneo la kiwanda umefikia asilimia 68%.  

 

Aliongeza kuwa, katika  kipindi cha robo ya pili ya Mwaka wa Fedha 2021/2022 kuna wazalishaji walioonesha nia ya kuwekeza katika uzalishaji wa mbolea ya asili  kwa kutumia majani na wadudu, na kubainisha kuwa  wazalishaji hao wapo  mikoa ya Morogoro na Mbeya ambapo tayari wameanza uzalishaji wa mbolea ya majaribio  na wanaendelea  na taratibu za usajili wa mbolea hizo.

 

Hizi ni baadhi ya jitihada zinazofanywa na  Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi mahiri wa Rais Samia Suluhu Hassan katika kutatua changamoto za wananchi wake hususani wakuliama ambapo asilimia 68 ya watanzania wameajiriwa katika sekta hiyo muhimu ya kilimo.

Share To:

Post A Comment: