Mkurugenzi wa Uzingatiaji na Utelezaji wa Sheria Bi. Redempta Samwel akitoa maelekezo kwa wafanyabiashara wa Soko la Machinga Jijini Dar Es Salaam, namna wanavyoweza kuitambua  mifuko na vifungashio visivyokua na viwango na vyenye viwango vinavyohitajika.
Mkurugenzi wa Uzingatiaji na Utekelezaji wa Sheria ya Mazingira Bi. Redempta Samwel akiwa ameambatana na watalaamu wengine kutoka NEMC wakifanya ukaguzi wa mifuko na vifungashio vya plastiki ambavyo havikidhi vigezo vinavyokubalika katika soko la Kisutu Jijini Dar es salaam.
 shehena ya viroba vyenye vifungashio visivyokidhi vigezo ambavyo vimekamtwa vikiwa vinauzwa katika maduka ya wafanyabiashara katika soko la Machinga Jijini Dar es Salaam.

****************

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limewaasa wananchi kutojihusisha na utengenezaji, usambazaji, uuzaji au utumiaji wa mifuko na vifungashio vya plastic visivyokidhi viwango kwa mujibu wa Sheria, kwani kufanya hivyo ni kosa la Kisheria.

Tamko hili limetolewa na Mkurugenzi wa Uzingatiaji na Utekelezaji wa Sheria Bi. Redempta Samwel kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa Baraza baada ya kufanya ziara ya kushtukiza katika soko la Kisutu na Machinga Jijini Dar es salaam.

 Katika ziara yake amebaini kuwa baadhi ya wafanyabiashara wasiowaaminifu wanajihusisha na uuzaji na usambazaji wa mifuko na vifungashio vya plastiki visivyokidhi vigezo.

 Bi. Redempta Samweli amesema baada ya kufanya ukaguzi, viroba zaidi ya hamsini vyenye vifungashio vya aina mbalimbali visivyokidhi viwango vimekamatwa na vitaharibiwa na hatua zaidi za Kisheria zitachukuliwa dhidi ya wanaohusika. 

Kufuatia changamoto hiyo, amewaambia watanzania kuwa ni marufuku kutengeneza, kusambaza, kuuza au kutumia mifuko na vifungashio hivyo, kwani kufanya hivyo ni kukiuka Sheria.

“Tumefanya kaguzi na kukamata viroba zaidi ya hamsini vyenye vifungashio vya aina mbalimbali vinavyotengenezwa hapa nchini visivyokidhi viwango. Viroba hivi vitaharibiwa na hatua kali za Kisheria zitachuliwa dhidi ya wanaohusika na zoezi hili ni endelevu. Kwa Sheria ya Mazingira na Kanuni ya kudhibiti mifuko ya plastiki ya mwaka 2019 ni marufuku kutengeneza, kusambaza, kuuza au kutumia vifungashio visivyokidhi viwango, kwani kufanya hivyo ni kukiuka Kanuni ya katazo la mifuko ya plastiki. Kwa yeyote atakayebainikana na kosa hilo tutamkamata na atachuliwa hatua za Kisheria.”

Sambamba na hilo Bi. Redempta Samwel, amewataka watanzanzania kuzingatia Sheria, Taratibu na Kanuni ili kuepuka migogoro na Serikali na kuepuka gharama zisizokua za lazima.

“Niwaombe watanzania wote kwa ujumla, tutumie mifuko mbadala na vifungashio vilivyoruhusiwa Kisheria na vyenye viwango ili kuepuka migogoro na Serikali na kupunguza gharama zisizokuwa za lazima.”

Naye Bw. Hamadi Taimuru Kissiwa Meneja Kanda ya Mashariki Kusini ameendelea kuwaasa wafanyabiashara na wananchi kwa ujumla kutokuzalisha, kutokupokea, kusambaza na kutumia mifuko na vifungashio visivyokuwa na viwango. 

Anasema watengenezaji wa vifungashio visivyokua na viwango hawalipi kodi na vifungashio hivyo vinauzwa kwa bei ya chini. Kufanya hivyo ni kuikosesha Serikali mapato na kudhoofisha biashara ya wananchi wanaotengenza mifuko na vifungashio kwa kuzingatia viwango.

“Tunawaasa wafanyabiashara na wananchi kwa ujumla wasinunue,wasitumie wala wasisafirishe na wasipokee kutoka kokote mifuko ambayo haikidhi viwango. Unaponunua bidhaa ambayo haijulikani inatoka wapi na inamana hata kodi ya serikali halipwi, bidhaa nyingine hazina viwango ina maana wale waliotekeleza viwango hawawezi kufanya biashara kwa sababu wafanyabiashara wanaotengeza bidhaa ambazo hazikidhi viwango watauza kwa bei ya chini hatimaye kuua soko la ushindani.”
Share To:

emmanuel mbatilo

Post A Comment: