Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Innocent Bashungwa amesema katika kipindi cha mwezi Julai hadi Disemba, 2021, Halmashauri zimekusanya jumla ya Sh bilioni 460.2 ambayo ni asilimia 53 ya makisio ya mwaka sawa na asilimia 107 ya lengo la nusu mwaka. 


Waziri Bashungwa amesema makusanyo ya mapato ya ndani ya Halmashauri katika kipindi cha miezi sita yameongezeka kwa Sh bilioni 78.9 ikilinganishwa na kipindi cha mwaka 2020.


Mhe. Bashungwa ameyasema hayo  jijini Dodoma hapa wakati wa taarifa za mapato na matumizi ya mapato ya ndani ya halmashauri kati ya Julai hadi Desemba mwaka 2021.


Alisema makusanyo ya halmashauri yaliyoongezeka ni sawa na ongezeko la asilimia 21. Kwa mwaka wa fedha 2021/22, Halmashauri zimepanga kukusanya Sh bilioni 863.9 kutoka kwenye vyanzo vyake vya ndani, bajeti hiyo ya imeongezeka kutoka Sh bilioni 814.96 katika mwaka wa fedha 2020/21 hadi Sh bilioni 863.9 katika mwaka wa fedha 2021/22


" Katika kipindi hiki Halmashauri za Wilaya za Kishapu na Longido zimeongeza jitihada katika ukusanyaji ukilinganisha na kipindi kama hiki cha mwaka wa fedha 2020/21 ambapo zilikuwa ni Halmashauri za mwisho kwa asilimia ya makusanyo. 


"Pia zipo baadhi ya Halmashauri ambazo katika kipindi cha Julai hadi Desemba mwaka 2021 ufanisi wa kukusanya umeshuka ukilinganisha na kipindi kama hiki cha Julai hadi Desemba mwaka 2020. Moja ya Halmashauri hizo ni Halmashauri ya Wilaya ya Masasi ambayo iliongoza kwa asilimia 88 na sasa imeshuka kwa asilimia 20."


Ofisi ya Rais - TAMISEMI ina utaratibu wa kutoa  taarifa ya ukusanyaji wa mapato kila robo mwaka ili kuongeza uwazi na uwajibikaji katika ukusanyaji wa mapato ya ndani ya Halmashauri Nchini. Taarifa hii ni ya kipindi cha nusu mwaka kwa mwaka wa fedha 2021/22

Share To:

Post A Comment: