Na Asila Twaha, TAMISEMI 


Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Elimu) Gelard Mweli amewataka wachezaji wa netiboli TAMISEMI QUEENS kuzingatia nidhamu na wacheze kwa kujituma katika kipindi chote cha michuano ya ligi ya netiboli ya Muungano.


Akizungumza  na wachezaji hao leo Jijini Dodoma wakati akiwaaga kuelekea Zanzibar  kushiriki ligi  mpira wa netiboli ya Muungano inayotarajia kuanza  kesho Januari 29, 2022 Mweli amesema kuwa,  nidhamu ndio msingi wa mafanikio  katika michezo hivyo amewataka  wachezaji hao  kuiwakilisha vyema Ofisi ya Rais –TAMISEMI katika nidhamu na ushindi.


 “Najua kombe tutachukua sababu sisi ni washindi kila siku  ila zingatieni nidhamu na uadilifu  katika kipindi chote cha michuano,  mkumbuke mnaiwakilisha Ofisi ya Rais -TAMISEMI, tunataka tusikie TAMISEMI Queens  sio kwamba inacheza vizuri tu  lakini pia kwa nidhamu inaongoza, nidhamu  ni sehemu ya ushindi” amesema Mweli. 


Aidha, ameupongeza uongozi wa  TAMISEMI Sports Club   kwa kujituma na  kuwekeza muda wao  ili  kuhakikisha timu hiyo inapata mahitaji yote muhimu  katika  ligi zilizopita na kuwataka    kuendeleza ari hiyo ili mafanikio hayo yawe endelevu.


“Niwapongeze viongozi mnaosimamia timu hii, mnajitoa sana nimeona katika ligi zilizopita umoja wenu na kujituma kwenu kumeleta matokeo mazuri katika timu yetu, niwaombe muendeleze ari hiyo” 

amesema Mweli


Pia amewahakikishia wachezaji wa Tamisemi Queens kuwa uongozi  wa Tamisemi unatambua jitihada zao katika michezo na wapo tayari kuhakikisha timu hiyo inafikia malengo walio jipangia.


 Naye Timu Kapteni Dafroza Luhwago ameushukuru uongozi wa Tamisemi kwa kuhakikisha timu hiyo inakuwa bora kwenye malezi ya kinidhamu na uchezaji pia ameahidi watarudi na ushindi.

Share To:

Post A Comment: