Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) limeendelea kuonesha uwezo wake wa kiteknolojia na uaminifu wa huduma zake katika Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa (Sabasaba) yanayoendelea katika Viwanja vya Mwalimu Nyerere, Dar es Salaam.

Kupitia kaulimbiu yao ya "TEHAMA SALAMA, TAIFA SALAMA", TTCL linajitambulisha kama mhimili wa maendeleo ya kidijitali nchini, likiwa na huduma mbalimbali bunifu zinazowawezesha wateja wa sekta zote kupata mawasiliano ya uhakika, salama na ya gharama nafuu.

Meneja wa Banda la TTCL, Bi. Janeth Maeda, amesema TTCL linashiriki maonesho hayo si kwa lengo la kibiashara pekee, bali pia kuelimisha jamii kuhusu nafasi muhimu ya Shirika hilo katika kusimamia miundombinu ya mawasiliano ya Taifa.



“Tuna dhamana ya kitaifa ya kusimamia Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano (NICTBB) na Kituo cha Taifa cha Kuhifadhi Data Kimtandao (NIDC). Huduma hizi ni msingi wa usalama wa taarifa na miundombinu ya TEHAMA nchini,” alisema Maeda.




Bi. Maeda alifafanua kuwa shirika hilo linatoa huduma kwa taasisi nyeti kama wizara, hospitali, mashule, taasisi za fedha, mashirika ya umma na sekta binafsi, kwa kutumia teknolojia ya fiber optic yenye kasi, uthabiti na usalama wa hali ya juu.

“Mashirika yanayotumia huduma za TTCL yameshuhudia kupungua kwa gharama za uendeshaji, ufanisi mkubwa katika utoaji wa huduma, na uimarishaji wa usalama wa taarifa,” aliongeza.

Katika msimu huu wa Sabasaba, TTCL linatoa ofasikabambe kwa wateja wake, ikiwa ni pamoja na punguzo maalum kwa vifaa vya mawasiliano kama vile routers, USB modems, na MiFi devices—ikiwa ni mkakati wa kusaidia wananchi kumiliki vifaa bora kwa urahisi zaidi.

Aidha, Bi. Maeda ametoa wito kwa washiriki wa maonesho, taasisi za ndani na nje ya nchi pamoja na wananchi kwa ujumla, kutembelea banda la TTCL namba 26 ili kujionea huduma za kisasa, kupata ushauri wa kitaalamu kuhusu TEHAMA, na kujifunza mbinu za kuongeza ufanisi wa kazi kwa njia za kidijitali.

“TTCL ni zaidi ya mtoa huduma; sisi ni sehemu ya maendeleo ya Taifa,” alisisitiza.

Share To:

OKULY BLOG

Post A Comment: