KATIBU Tawala Mkoa wa Arusha, Dkt. Athumani Kihamia ameeleza kuwa mara ya kwanza nchi tangu imepata Uhuru imeweka historia ya uwazi na uwajibikaji wa fedha zilizokopwa nje ya nchi kwa masharti nafuu.

Akizungumza nasi kupitia njia ya simu amesema ni jambo la kumshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuweka uwazi wa mkopo wa Sh. trilioni 1.3 na wananchi kujua namna ilivyotumika kwa fedha hiyo.

Ameendelea kueleza kuwa mataifa na nchi nyingi duniani zilizopiga hatua kimaendeleo ndizo hizo zinazoongoza kwa kukopa zaidi katika taasisi za kifedha za kimataifa.

“Nchi hizo hizo zinazoongoza kwa kukopa ndizo zinazoongoza kuwekeza kwenye miradi ya kimkakati ambayo huwa inazalishaf kubwa na kuchochea kasi ya maendeleo endelevu,” alisema.

Alisema miongoni mwa nchi hizo ni Japan, Marekani, Ufaransa, Uingereza na Tanzania chini ya Rais Samia kwa sasa imezinduka usingizini na imechungulia mbali na kugundua ujanja wa mataifa makubwa, ambapo sasa na yenyewe imeamua kwenda sambamba na mataifa haya yaliyofanikiwa kwa kuiendeleza miradi ya kimkakati kwa kasi kubwa.

Miradi hiyo ikiwemo ujenzi wa miundo mbinu ya reli, bandari, bwawa kubwa la umeme, miundombinu ya afya, elimu,barabara, mabomba ya mafuta, utalii, maji na anga.Hii ni hatua kubwa ya kupongezwa kwa serikali ya awamu ya sita.

Dkt.Kihamia alisema kuna uhusiano mkubwa wa faida (positive correlation) kati ya maendeleo na mikopo katika mataifa hayo makubwa.

“Jambo la kushangaza Afrika nzima kwa ujumla imekopa asilimia 2 tu ya deni lote la dunia huku Marekani pekee ikiwa na asilimia 31.8 ya deni lote la dunia,” alisema.

Dkt. Kihamia alisema kuna umuhimu wa kumuunga mkono Rais Samia azidi kuharakisha maendeleo.

“Tuwe macho na wazalendo wa kweli dhidi ya baadhi ya wenzetu wachache wenye nia na malengo hasi dhidi ya kasi ya maendeleo,” alisema.

Alisema jambo la muhimu ni usimamizi madhubuti wa utekelezaji wa miradi hiyo ya kimkakati ambayo inasimamiwa kwa uwazi.

“Shukrani zimuendee Rais Samia na viongozi waandamizi wanaomsaidia kwa kuainisha kwa uwazi fedha za mikopo zinakoelekezwa watanzania wengi zaidi wameridhishwa na mchanganuo wa matumizi ya fedha hizo ambapo kila mkoa, wilaya na Halmashauri zimeguswa na mgao huo kulingana na mahitaji halisi,” alisema.

Alisema kitendo cha kuwa waoga na kuchelewa kukopa kwa masharti nafuu kwa waafrika ni kuendekeza umaskini.

Aidha, alisema kwa upande wa Mkoa wa Arusha kazi zinaendelea na zinaonekana.Baada ya miaka michache ijayo watashuhudia Tanzania yenye neema zaidi.

Share To:

Post A Comment: