Na. Tito Mselem, Morogoro


Imeelezwa kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Rais wa Serikali ya Awamu ya Sita Samia Suluhu Hassan inawadhamini na kuwatambua Wajiolojia kwa juhudi wanazo zifanya za kuleta maendeleo ya Kiuchumi Nchini.


Hayo yamebainishwa na Naibu Waziri wa Madini Prof. Shukrani Manya wakatI akifungua Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Wajiolojia Tanzania (TGS) 2021 uliofanyika katika ukumbi wa Nashera uliopo Mkoani Morogoro.


Prof. Manya amesema, taaluma ya Jiolojia Nchini inatambuliwa na inadhaminiwa kwa kuwa ni mmoja kati ya fani zinazo husisha shughuli za aina nyingi zenye kuchochea Maendeleo mbalimbali ya kiuchumi na jamii ulimwenguni kote.


Aidha, Prof. Manya amewataka wajumbe wa Jumuiya ya Wajiolojia nchini kuhakikisha wanabadilishana taarifa na uzoefu ili kujijengea uwezo katika taaluma yao kuliko kukaa na kusubiri Mkutano Mkuu ambao hutokea mara moja kwa Mwaka.


“Kama kuna jambo lolote la kijiosayansi hakikisheni mnashea taarifa ili kujijengea uelewa, mfano kuna watu hapa nawafahamu wamekaa Ghana, Mali na kwingine lakini hawatoi uzoefu walioupata huko walipo kuwa hii sio sawa, inatakiwa tuyashee yale tuliyojifunza huko ili tuiimarishe fani yetu ya Jiosayansi,” amesema Prof. Manya.


Pia, Prof. Manya amesema kipindi cha nyuma Sekta ya Madini ilikuwa haikopeshwi na benki, lakini baada ya Tume ya Madini kutoa Semina kwa benki mbalimbali Nchini, sasa Mikopo inatolewa kwa wachimbaji na wafanyabiashara ya madini.


Sambamba na hilo, Prof. Manya amewataka wadau wote wa Jumuiya hiyo kuhakikisha wanatoa maoni yao ili liandikwe andiko kwa Baraza la Mawaziri kwa lengo la kuomba kibali cha kuanzisha bodi ya Wajiolojia itakayo kuwa inasimamia weledi wa taaluma ya wajiosayansi na kuwatambua kisheria.


Sambamba na hilo, Prof. Manya amekabidhi tuzo za heshima kwa baadhi ya washiriki wa Mkutano huo ambapo Tume ya Madini na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) ni miongoni mwa Taasisi za Serikali zilizokabidhiwa tuzo ya heshima iliyo andaliwa na Jumuiya hiyo.


Awali Prof. Manya, alitia nanga kwa Mkuu wa Wilaya ya Morogoro Albert Msando na kupatiwa taarifa za shughuli za Sekta ya Madini ya Mkoa wa Morogoro ambapo aliwasisitiza Wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama wa Wilaya hiyo kuendelea kusimamia Shughuli za Sekta ya Madini.


Kwa upande wake, Rais wa Jumuiya ya Wajiolojia Nchini, Prof. Abdukarim Mruma amemuamba Naibu Waziri Prof. Manya kusimamia mchakato wa kuanzisha Bodi ya Usajili wa Wajiosayansi utakao saidia kusimamia weledi wa taaluma ya jiosayansi Nchini kupitisha taarifa na maandiko mbalimbali ya wataalamu wa jiosayansi.


Prof. Mruma amesema lengo la Mkutano wa Jumuiya hiyo ni kujadili hatima ya umoja wao pamoja na kukumbushana majukumu yao wanayotakiwa kuyafanya ili kuchochea Maendeleo Taifa.


Katika hatua nyingine, Prof. Mruma amesema, Mchango wa Sekta ya Madini, Nishati na Maji Ardhi umekua kwa kiwango kikubwa ambapo Wajiosansi wanahusika kwa kiwango kikubwa katika kuchochea ukuaji huo.


Mkutano Mkuu wa Jumuiya ya Wajiolojia Tanzania (TGS) hufanyika kila Oktoba ya kila Mwaka ambapo Mkutano wa Mwaka 2021 umebebwa na Kauli Mbiu isemayo “Sera Bora kwa Maendeleo Endelevuya ya Sekta ya Uziduaji”.

Share To:

Post A Comment: