Nteghenjwa Hosseah, OR-TAMISEMI


SERIKALI iko kwenye mchakato wa kuangalia gharama za uendeshaji wa halmashauri zote Nchini ili kuja na muongozo wa matumizi ya Fedha za uendeshaji wa halmashauri.


Haya yameelezwa jijini hapa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mhe. Ummy Mwalimu wakati wa kufunga mkutano wa Jumuiya ya Tawala za mitaa unaojumuisha mameya,wenyeviti wakurugenzi wa halmashauri, miji, manispaa na majiji.


Mhe. Ummy alibainisha hayo kufuatia ombi la Mwenyekiti wa Jumuiya ya Mamlaka za Mitaa Mhe. Murshid Ngeze ambaye aliiomba Serikali kuangalia mgawanyo wa fedha za mapato ya ndani kwa Uendeshaji wa Halmashauri na zile zinazopelekwa kwenye Utekelezaji wa miradi  ya maendeleo.


Alisema kutokana na mgawanyo huo imekuwa vigumu Kwa halimashauri kujiendesha hasa kwa zile Halmashauri zenye mapato madogo.

 

Akifafanua, Mhe. Ummy amesema maelekezo ya kupeleka asilimia 40 Kwa halmashauri zenye mapato kidogo na asilimia 60 kwa halmashauri zinazokusanya zaidi ya Sh bilioni 5 utaendelea kutekelezwa na kusimamiwa.


Hata hivyo, alisema kamati inayoongozwa na Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais-TAMISEMI inapitia na kuangalia tena gharama za Uendeshaji katika halmashauri zote zenye mapato makubwa na zile zenye mapato kidogo ili baadaye kuja na muongozo wa namna bora ya matumizi ya fedha za uendeshaji.


“Tumeangalia gharama za  posho za kamati za kudumu za Halmashauri, vikao na ufuatiliaji wa miradi, posho za mwezi kwa zile Halmashauri zinazolipa, uendeshaji wa ofisi za kata na vijiji, wenyeviti mitaa, posho za wenyeviti wa halmashauri, kata pamoja na matumizi mengineyo.


“ Pia posho za wakuu wa idara na vitengo, posho za watendaji wa kati, watumishi wa mikatataba, vikao vya kisheria na mabaraza hivyo tunakuja na muongozo wa utakaobainisha kiasi cha fedha za kuendesha Halmashauri zenye mapato ya chini sambamba na zile zenye mapato makubwa.


Maana unaweza kuangalia ukakuta  Halmashauri inakusanya Shilingi Bilioni 5 gharama sa uendeshaji ni shilingi Bilioni 2 lakini kuna halmashauri inayokusanha shilingi Mil 600 na gharama ya uendeshaji ni shilingi Mil 360 tu unajiuliza hawa wanawezaje kundesha Halmashauri kwa milioni mia tatu ili hali wengine wanaendesha kwa bilioni mbili hivyo lazima tutoe muongozo hata kama una mapato makubwa tufahamu hizo fedha zinatumikaje alisisitiza Waziri Ummy.


Ummy aliongeza:” Tunataka kuona fedha za mapato zinakwenda kuleta maendeleo, shida za wananchi zinatatuliwa, lakini pia tutahakikisha maslahi yenu yanazingatiwa na wakati huo huo   fedha zinarudi kwa wananchi kwa njia ya maendeleo.


Alisema ni muhimu kwa Mameya, Wenyeviti na Wakurugenzi kuhakikisha wanakusanya mapato  ipasavyo na kusisitiza kuwa endapo halmashauri haitafanya vizuri katika eneo la ukusanyaji wa mapato basi Mkurugenzi atakuwa hatoshi katika hiyo nafasi.


Pia aliwataka kuhakikisha wanaongeza usimamizi wa fedha zinazopelekwa kwenye maeneo yao kwa ajili ya miradi ya maendeleo ikiwa ni pamoja na elimu, afya, barabara na kuwezesha wananchi kiuchumi kuanzia ngazi ya chini.


Aidha Ummy amesisitiza wakurugenzi, wenyeviti na mameya wa halmashauri kuhakikisha wanatekeleza maagizo na maelekezo yaliyotolewa na Rais Samia Suluhu Hassan wakati awakati alipofungua mkutano huo.

Share To:

Post A Comment: