Na Mwandishi Wetu- Dar e's Salaam.


Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Zainabu Chaula, amekutana na kufanya mazungumzo na baadhi ya Wakuu wa Mashirika na Taasisi mbalimbali zinazotoa huduma ya kiserikali kwa jamii. 


Kikao hicho kimefanyika leo tarehe 6 Julai 2021, huku kikihudhuriwa na Wakuu wa Taasisi mbalimbali kutoka Wakala wa Usajili Ufilisi na Udhamini (RITA), Mamlaka ya vitambulisho vya Taifa(NIDA), Wakala ya Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Bima ya Afya (NSSF), UHAMIAJI na Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma. 


Kikao hicho kilienda sambamba na kuitambulisha huduma mpya ya kiteknolojia iitwayo "HUDUMA PAMOJA CENTER", ambayo itakuwa ikifanya kazi ya kutoa huduma mbalimbali za kiserikali mahala pamoja na kwa ukaribu zaidi na Jamii kupitia ofisi za Posta, Tanzania nzima. 


Dkt. Chaula alieleza huduma zitakazokuwa zikipatikana kwenye kituo hicho kuwa ni vyeti vya kuzaliwa na vifo, utoaji wa Passports ndogo, Utoaji wa Kitambulisho cha Taifa(NIDA), usajili wa Biashara mbalimbali kupitia BRELA, utoaji wa TIN namba, Leseni za Biashara pamoja na Usajili wa wanachama wapya wa NSSF.


Katibu Mkuu aliwataka wanahabari kutangaza huduma hii kwa jamii, huku Kaimu Postamasta Mkuu wa Shirika la Posta Tanzania, Bwana Macrice Mbodo akitoa wito kwa Wananchi wote kujitokeza kwa wingi kwa ajili ya kupata huduma katika Vituo hivi vilivyoanza kutoa huduma tarehe 1 Julai, 2021 ambavyo viko katika ofisi za Posta Kuu Dar es Salaam (GPO) na Posta Kuu Dodoma.

Share To:

Post A Comment: