Spika wa Bunge,  Job Ndugai leo Jumanne Juni Mosi,  2021  amemtoa katika ukumbi wa Bunge  mbunge wa Momba (CCM),  Condester Sichwale kutokana na kuvaa suruali iliyombana.

Kwa mujibu wa kanuni za Bunge,  wabunge wanawake hawaruhusiwi kuvaa suruali za kubana.

Mara baada ya kipindi cha maswali na majibu, alisimama mbunge wa Nyang'wale (CCM),  Hussein Amar na kuomba mwongozo wa Spika.

"Spika nasimama kwa kanuni ya  70 inayohusu mavazi ya staha kwa wabunge, kanuni imeeleza  wazi kuhusu mavazi hayo na kwa akina dada lakini humu ndani kuna wabunge wamevaa nguo ambazo hazina staha," amesema Amar.

Spika Ndugai alimpa nafasi mbunge huyo kumtaja mwenzake  aliyevaa mavazi ambayo hayakuwa na staha ili iwe mfano.

"Mbunge huyo yuko hapo katika mkono wangu wa kulia, amevalia tisheti  lakini naomba umuite mbele uone suruali aliyovaa namna ilivyobana, amevaa miwani," amesema Ameir bila kumtaja jina.

Spika alisimama na kumtaka mbunge aliyevaa mavazi hayo asimame na aondoke ndani ya ukumbi ili akavae mavazi yenye staha ndipo atarejea tena bungeni.

Sichwale alisimama  akabeba mkoba wake na  kutoka nje ya ukumbi wa Bunge.

Spika Ndugai ameagiza askari wote katika milango ya kuingia bungeni wawe makini wasiruhusu wabunge kuingia wakiwa wamevaa mavazi yaliyokatazwa.

Share To:

msumbanews

Post A Comment: