Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini  Mh. Anthony Mavunde ameanza kuboresha miundombinu ya viwanja vya michezo katika shule za Msingi na Sekondari za Jiji la Dodoma kwa kulenga la kukuza michezo na kuwaandaa wanafunzi wenye vipaji kuanzia ngazi ya chini.


Mbunge Mavunde ameyasema hayo leo katika shule ya Sekondari Dodoma wakati akikabidhi vifaa vya michezo vyenye thamani ya Tsh 3,000,000 kwa wanafunzi wanaounda Timu ya Jiji la Dodoma katika mashindano ya UMISETA ngazi ya Mkoa,ambapo amewahakikishia wanafunzi hao kuwawekea miundombinu bora katika viwanja vya shule zao wanavyotumia kwa ajili ya michezo mbalimbali.


“Nimefurahi kujumuika hapa nanyi siku ya leo ikiwa ni hafla fupi ya kuwakabidhi vifaa vya michezo na kuwatakia kila la kheri katika mashindano yenu ya UMISETA ngazi ya mkoa.


Ningependa kuona Jiji la Dodoma linakuwa mbele katika kila jambo ikiwemo michezo,hivyo ni imani yangu kwamba mtafanya vizuri katika mashindano haya ya mkoa.


Ninaendelea kuboresha miundombinu ya viwanja katika shule zenu kwa kuweka magoli ya chuma na kukarabati baadhi ya viwanja.Awamu ya kwanza naanza na Shule 20 za msingi na Sekondari na baadaye tutamalizia katika viwanja vilivyobaki”Alisema Mavunde


Wakati huo huo,Mh Mavunde alitumia fursa hiyo kuwatakia kila la kheri Timu ya UMITASHUMTA ya mkoa wa Dodoma ambayo inajiandaa na safari ya kuelekea Mtwara kushiriki mashindano ya UTAMITASHUMTA ngazi ya Taifa na kuwaahidi kiasi cha Tsh 2,000,000 wakishinda michezo mitano.


Akishukuru kwa niaba,Afisa Elimu wa Sekondari Jiji la Dodoma Mwl. Upendo Rweyemamu amemshukuru Mbunge Mavunde kwa kufadhili vifaa vya michezo kwa Timu za Wanafunzi za Jiji la Dodoma kila mwaka na kumuahidi ushindi katika michezo yote ili kulinda heshima ya Jiji la Dodoma katika ngazi ya mkoa.

Share To:

msumbanews

Post A Comment: