#Yatenga Bilioni 133 kukopesha Wachimbaji


*Na Asteria Muhozya, Dodoma*


Siku moja tu baada ya Waziri wa Madini Doto Biteko kuzindua Jukwaa la Madini la Benki ya NMB kwa Mkoa wa Dodoma, Benki hiyo imezidi kupiga hodi Sekta ya Madini ili kuhakikisha wadau wa madini hususan wachimbaji wadogo wananufaika ipasavyo na huduma zinazotolewa na benki hiyo ikiwemo mikopo.


Leo Juni 29, 2021, Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini Prof. Simon Msanjila amekutana na ujumbe wa Benki hiyo ukiongozwa na Mkuu wa Kitengo cha  Biashara Alex Mgeni katika kikao kilichofanyika Makao Makuu ya Wizara , jijini Dodoma kikilenga kuweka mikakati zaidi ya kuwasaidia wachimbaji wadogo nchini kupitia benki hiyo.


Aidha, pamoja na masuala kadhaa yaliyojadiliwa, Prof. Msanjila amepokea mrejesho wa baadhi ya changamoto zilizoibuliwa na wadau baada ya benki hiyo kufanya Kongamano la Siku moja lililokwenda sambamba na uzinduzi wa jukwaa la madini huku dhamira ya kuwasilisha changamoto hizo ikiwa ni kuweka mkakati madhubuti wa pamoja na serikali wa namna bora ya kutatua changamoto hizo ili kuwawezesha wachimbaji kunufaika na huduma za mikopo zinazotolewa na benki hiyo.


Prof. Msanjila amezitaka taasisi za kifedha kuongeza kasi ya kubaini fursa za kibiashara zilizopo katika sekta ya madini na kuzitumia ikiwemo kujifunza namna mifumo ya uchimbaji madini hususani ya wachimbaji wadogo inavyofanya kazi.


‘’Kuna biashara nyingi migodini, tafuteni muda wa kuisoma Sekta ya madini, mtumie fursa za kibiashara zilizopo’’ amesema Prof. Msanjila.


Pia, amezitaka taasisi za kifedha kuweka mazingira rafiki ya kibiashara yatakayowawezesha wawekezaji katika Sekta ya Madini kuweza kukopa kupitia benki za ndani.


Akizungumzia vipaumbele vya wizara, amesema miongoni mwa maeneo hayo ni kuifungamanisha Sekta ya Madini na Sekta nyingine za kiuchumi huku akizitaja taasisi za kifedha kuwa mdau muhimu wa kuwezesha utekelezaji wa kipaumbele hicho.


Kwa upande wake, Mkuu wa  Kitengo cha Biashara Alex Mgeni amesema kuwa, Mabadiliko yaliyofanyika katika Sheria ya Madini yameipa nguvu benki hiyo kujikita katika Sekta ya Madini ambapo kuanzia mwaka 2020 benki imetoa mkopo  wa kiasi cha shilingi bilioni 63 kwa wachimbaji wadogo, vilevile ikiwa imetoa mkopo wa kampuni ya uchimbaji mkubwa wa madini ya Geita.


Ameongeza kuwa, mbali na kutoa mikopo, benki hiyo imetoa mafunzo kwa wachimbaji wadogo ili waweze kufahamu biashara za kibenki zinazotolewa na NMB.


 Vilevile amesema kuwa, mbali na kuanzisha jukwaa la madini katika mkoa wa Dodoma, pia, imepanga kuanzisha majukwaa ya madini katika mikoa ya Mwanza, Arusha, Morogoro na Mbeya.


Naye, Meneja Mwandamizi Wateja  Wakubwa wa Benki hiyo Amour Muro,  amesema kwa mwaka huu benki hiyo imetenga kiasi cha shilingi bilioni 133 kwa ajili ya kutoa mikopo kwa wadau wa Sekta ya Madini na kuongeza kuwa, uwezo wa kutoa  mikopo kwa wachimbaji upo.


‘’Katibu Mkuu haya yanafanyika kutokana na mabadiliko yaliyotokea kwenye Sheria ya Madini lakini pia ushirikiano tunaoupata wa wizara na taasisi zake mfano RMO wa Dodoma amesaidia sana kuwafundisha Maafisa wetu wa Benki kuhusu masuala haya ya sekta ya madini,’’ amesema Muro.

Share To:

msumbanews

Post A Comment: