chongo mkubwa. Jisajili sasa!


Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula (Mb) amekutana na kuzungumza na mabalozi wanne wanaowakilisha nchi zao hapa nchini na kupokea nakala ya hati ya utambulisho ya balozi mteule wa Msumbiji hapa nchini.

Mabalozi waliokutana na Waziri katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam ni Balozi wa Rwanda, Mhe. Meja Jenerali Charles Karamba, Balozi wa Indonesia Mhe. Ratlan Pardede, Balozi wa Sweden Mhe. Anders Sjöberg na Balozi wa Norway Mhe. Elisabeth Jacobsen.

Pamoja na mambo mengine, Mhe. Waziri Mulamula na mabalozi hao wamejadili juu ya kuimarisha na kuongeza ushirikiano baina ya mataifa wanayoyawakilisha hapa nchini na Tanzania.    

 “Leo nimekutana na mabalozi kadhaa wanaowakilisha nchi zao hapa nchini, akiwemo Balozi wa Rwanda, Sweden, Norway na pia nimepokea nakala ya hati ya utambulisho ya balozi mteule wa Msumbiji na kuwahakikishia ushirikiano wetu kama wizara, kama nchi katika kuboresha na kukuza mahusiano yetu,” amesema Balozi Mulamula

Nae Balozi wa Rwanda hapa nchini, Mhe. Meja Jenerali Charles Karamba amesema kuwa ushirikiano baina ya Tanzania na Rwanda ni mzuri hivyo wataendelea kuudumisha uhusiano huo kwa maslahi ya pande zote mbili.

“Nchi zetu mbili zimekuwa zikishirikiana vizuri hivyo tumekubaliana kuendelea kudumisha ushirikiano huu kwani Watanzania na Wanyarwanda ndugu na marafiki,” amesema Balozi Karamba

Kwa upande wake Balozi wa Indonesia hapa nchini Mhe. Ratlan Pardede amesema Indonesia na Tanzania zitaendelea kushirikiana katika mambo mbalimbali ikiwemo uchumi, utalii na kijamii na kuhakikisha kuwa ushirikiano huo unazidi kuimarika.

“Tumejaribu kuwahamasisha wawekezaji kutoka Indonesia kuja kuwekeza hapa Tanzania na hadi sasa kampuni kumi (10) zimewekeza katika sekta za biashara na uwekezaji, madini, uvuvi, ujenzi na viwanda,” amesema Balozi Pardede     

Nae Balozi wa Sweden Mhe. Anders Sjöberg amesema kuwa Sweden itaendelea kuimarisha mahusiano na ushirikiano katika sekta za biashara na uwekezaji, utunzaji wa mazingira na masuala ya kijamii kama vile usawa wa kijinsia, uhuru wa vyombo vya habari pamoja na haki za binadamu.

“Tumejadiliana kuhusu kuimarisha mahusiano, biashara na uwekezaji, utunzaji wa mazingira pamoja na masuala ya kijamii kama vile usawa wa kijinsia, uhuru wa vyombo vya habari na haki za binadamu,” amesema Balozi Sjöberg.

Kwa upande wake Balozi wa Norway hapa nchini, Mhe. Elisabeth Jacobsen amesema Norway na Tanzania zimekuwa na uhusiano mzuri ambapo kwa sasa Norway inaangalia fursa za uwekezaji na biashara hapa nchini ili kuimarisha mahusiano na kukuza uchumi.

“Norway itaendela kutumia fursa za uwekezaji na biashara zilizopo Tanzania ili kuimarisha mahusiano yetu na kukuza uchumi wa pande zote mbili,” amesema Balozi Jacobsen

Katika tukio jingine, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula (Mb) amepokea nakala ya hati ya utambulisho kutoka kwa Balozi Mteule wa Msumbiji hapa nchini Mhe. Ricardo Ambrosio Sampaio Mtumbuida.
Share To:

Post A Comment: