Na. Elizabeth Joseph,Shinyanga.


Halmashauri za Mkoa wa Shinyanga zimepokea fedha kiasi cha shilingi milioni 167.4 pamoja na kinga tiba kwa ajili ya zoezi la ugawaji wa kinga tiba kwa watoto wenye umri wa kwenda shule linalotarajiwa kuanza mwishoni mwa mwezi Mei mwaka huu.


Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Bi, Zainab Telack aliyasema hayo leo wakati wa kufungua kikao kazi cha uraghibishaji na uhamasishaji wa magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele kilichoandaliwa na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Wazee na Watoto kupitia Mpango wa Kudhibiti Magonjwa Yaliyokuwa Hayapewi Kipaumbele.


Alisema kuwa Mkoa wake umejipanga vizuri  kwa ajili ya kutekeleza zoezi hilo kwa wanafunzi wote wenye umri wa miaka mitano hadi kumi na nne hivyo kuwataka Wakurugenzi wa halmashauri zote mkoani humo kuhakikisha zoezi la ugawaji wa kinga tiba za Kichocho na Minyoo ya tumbo linafanikiwa ili kudhibiti magonjwa hayo.


“Magonjwa haya yameathiri jamii yetu na kuleta ulemavu hali ambayo  imeleta usumbuvu kwa wananchi na watoto kutokuweza kuhudhuria vizuri masomo yao vizuri na kupunguza rasiliamali chache tulizonazo”.aliongeza Mkuu huyo.


Aidha Bi,Telack amewataka wananchi wenye Imani potofu juu ya Kinga hizo kuondoka dhana hiyo na kuwahakikishia kwa kusema kuwa kinga tiba hizo ni salama na zimethibitishwa  na Shrika la Afya Duniani(WHO) na Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba Tanzania (TMDA).


Aliongeza kwa kuwataka wataalam wa afya na elimu kuwaeleimisha wananchi kwenye maeneo yao kwa kuwapa ujumbe sahihi ili itakapofika wakati wa zoezi hilo kusaidia kutokomeza tatizo hilo mkoani humo.


Kwa upande wake Ofisa Mradi kutoka Mpango wa Kudhibiti Magonjwa Yaliyokuwa hayapewi Kipaumbele,Wizara ya afya Bw,Isaac Njau alisema zipo athari nyingi za muda mfupi na mrefu zitokanazo na kichocho kwa wanaume, wanawake na watoto ikiwemo Udumavu, utapiamlo, kuvimba Ini, kuharibika kwa mimba, Kanda ya kibovu Cha miojo pamoja na upungufu wa Damu mwilini.


Njau aliyataja Magonjwa Yaliyokuwa Hayapewi Kipaumbele  ni pamoja na Usubi,Trackoma,Kichocho,Minyoo ya Tumbo,Matende na Mabusha(Ngirimaji).


Share To:

msumbanews

Post A Comment: