Na Mwandishi wetu,Geita


Imeelezwa kuwa, kufuatia Kuanzishwa kwa Kiwanda cha Kusafisha Madini ya Dhahabu cha Geita Gold Refinery (GGR) cha Mkoani Geita, kitaongeza na kuchangamsha uchumi wa Mkoa na Taifa kwa ujumla.


Hayo yamesemwa na Waziri wa Madini  Doto Biteko  Mei 8 2021, wakati akiweka Jiwe la Msingi katika kiwanda hicho wakati wa  ziara ya kikazi Mkoani Geita.


Waziri Biteko alisema kuwa kiwanda hicho cha kisasa na cha kwanza cha aina yake barani Afrika kimekusudia kuimarisha nyanja za kusafisha dhababu nchini jambo litakaimarisha soko la uhakika la uuzaji wa madini na kuiwezesha Benki Kuu kununua madini yenyewe.


Alisema kuwa,  uwepo wa kiwanda hicho ni fahari kubwa katika Sekta ya Madini kwani uwekezaji huo ni mkubwa na muhimu utakaojibu ndoto za serikali katika kuwakomboa wachimbaji wadogo wa madini.


Waziri Biteko aliwaasa wachimbaji kuwa na ushirikiano na kupendana kwani uchumi wa nchi hauwezi kuimarika kwa baadhi ya wachimbaji kuwachukia waliofanikiwa.


“Nasikitika kuna vijiwe vimegawanyika kazi yao kusuka majungu na kuwachukia wengine waliofanikiwa, Ushindeni ubaya kwa wema, aliyefanikiwa tumuombee Mungu amsogeze mbele” amekaririwa Waziri Biteko.


Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhandisi Robert Gabriel  alisema kuwa, dhahabu inayouzwa katika mkoa huo imeamsha ari kwa wawekezaji kuanza kuwekeza katika sekta mbalimbali jambo linaloimarisha uchumi wa mkoa.


Alisema kuwa,  mkoa wa Geita pamoja na mambo mengine  ni sehemu sahihi kwa ajili ya kuwekeza katika sekta ya madini.


Awali, akisoma taarifa ya kiwanda cha kusafisha madini cha GGR Kaimu Mkurugenzi wa Bodi Mhandisi Athuman Mfutakamba alisema kuwa kiwanda hicho kilipewa leseni ya kusafisha dhahabu No RFL 001/2019 iliyotolewa na Wizara ya Madini tarehe 16 Julai 2019 na kina uwezo wa kusafisha 400 kg kwa siku na kufikia tani 200 kwa mwaka kwa kiwango cha juu kabisa na kukidhi kufikia kiwango cha usafi wa asilimia 999.9 na 999.5.


Alisema kampuni imejiimarisha ipasavyo kutekeleza wajibu huo kwa kufunga vifaa/mashine za kusafisha dhahabu vya kisasa na vyenye viwango vya hali ya juu vinavyokidhi viwango vya kimataifa.

Share To:

msumbanews

Post A Comment: