Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Prof. Mohamed Janabi akizungumza na waandishi wa habari kuhusu upasuaji wa moyo wa bila kusimamisha moyo uliofanywa na wataala wa afya wa JKCI kwa kushirikiana na Daktari bingwa wa upasuaji wa moyo na mishipa ya damu Subhash Sinha (kushoto) kutoka hospitali ya Max iliyopo New Delh nchini.

Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Upasuaji wa moyo na mishipa ya damu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Angella Muhozya katika picha ya pamoja na wataalam wa afya wanaofanya kazi katika chumba cha upasuaji wa moyo na chumba cha wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalum (ICU) baada ya kikao cha tathmini ya kambi maalum ya upasuaji wa moyo wa bila kusimamisha moyo Iliyofanywa na wataalam hao kwa kushirikiana na Daktari bingwa wa upasuaji wa moyo na mishipa ya damu Subhash Sinha (kushoto aliyekaa) kutoka hospitali ya Max iliyopo New Delh nchini.


Wagonjwa 22 wamefanyiwa upasuaji wa moyo wa kupandikiza mishipa ya damu kwenye moyo wakati moyo ukiwa unafanya kazi katika kambi maalum ya matibabu ya siku kumi iliyofanywa na madaktari wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete kwa kushirikiana na Daktari bingwa wa upasuaji wa moyo na mishipa ya damu Subhash Sinha kutoka hospitali ya Max iliyopo New Delh nchini India.

Upasuaji huo umegharimu kiasi cha shilingi milioni 330 ambapo kama wagonjwa hao wangepelekwa nje ya nchi kwa ajili ya matibabu hayo gharama za matibabu zingefikia kiasi cha shilingi milioni 900.

Akizungumza na waandishi wa habari hivi karibuni kuhusu kambi hiyo Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI Prof. Mohamed Janabi amesema JKCI imekua ikifanya kambi mbalimbali za matibabu na wataalam kutoka nje ya nchi kwa lengo la kubadilishana uzoefu na kupata mbinu mpya za kitabibu.

“JKCI tumekua tukifanya upasuaji wa kupandikiza mishipa ya damu kwenye moyo takribani miaka mitano lakini tofauti kubwa ni kwamba sisi tulikua tunasimamisha moyo kabisa ndio tunafanya upasuaji na baada ya hapo tunaustua moyo lakini kupitia ujuzi tulioupata kutoka kwa Daktari kutoka Hospitali ya MAX Subhash Sinha tumeweza kupandikiza mishipa ya damu kwenye moyo bila kuusimamisha moyo” alisema Prof. Janabi

“unapofanya upasuaji wa moyo wa kupandikiza mishipa ya damu wakati moyo unapiga humsaidia mgonjwa kukaa muda mfupi zaidi hospitali, hatari za upasuaji zinakua chache zaidi, upasuaji unatumia muda mfupi tofauti na ule wa kuusimamisha moyo lakini pia mgonjwa hutumia siku 10 hadi 14 kurejea katika hali yake ya kawaida na kuendelea na shughuli zake” alisema Prof. Janabi

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Upasuji wa Moyo na Mishipa ya Damu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete Angella Muhozya amesema Kuwa kwa kipindi cha miaka mitano JKCI imefanya upandikizaji wa mishipa ya damu kwenye moyo kwa wagonjwa zaidi ya 100.

“Utaalamu huu tulioupata kutoka kwa Dkt. Sinha wa kupandikiza mishipa ya damu kwenye moyo bila ya kuusimamisha moyo utatusaidia kuwafanyia upasuaji wagonjwa wengi zaidi kwa kipindi kifupi tofauti na awali tulipokua tukisimamisha moyo kwani ilitulazimu kuchukua muda mwingi kufanya upasuji huo” alisema Dkt. Angella

 “Baada ya kambi hii sisi kama JKCI tutaendelea kufanya upasuaji huu kwa wagonjwa wetu bila kusimamisha moyo lengo letu likiwa ni kuifanya JKCI kuwa kituo cha ubora katika kutoa huduma za matibabu ya afya ya moyo” alisema Dkt. Angella

Naye Daktari bingwa wa upasuaji wa moyo na mishipa ya damu Subhash Sinha kutoka hospitali ya Max iliyopo New Delh nchini India amewapongeza wataalam wa afya wa JKCI kwa huduma bora za kitatibu wanazozitoa kwa wagonjwa wao huku akiwataka wataalam hao kuendelea kujifunza kila wanapopata nafasi ya kujifunza mbinu mpya za kitabibu.

“Madaktari wa JKCI wana utayari wa kujifunza na kubadilishana uzoefu nasi, hii nimeiona nilivyokuwa nafanya nao upasuaji kwa kipindi cha siku hizi 10, naamini JKCI inaelekea kuwa tegemeo barani Afrika kutokana na huduma bora na nzuri wanazozitoa” alisema Dkt. Sinha.

Share To:

Post A Comment: