Wanachama 25 wa Chama cha Mapinduzi CCM, wamejitokeza kuchukua fomu za kuwania ubunge katika Jimbo la Muhambwe Wilaya ya Kibondo Mkoani Kigoma ili kujaza nafasi iliyoachwa wazi na aliyekuwa mbunge wa Jimbo hilo Marehemu Mhandisi Atashasta Nditiye aliyefariki dunia kwa ajali Februari 12 mwaka huu jijini Dodoma.

Kaimu katibu wa CCM wilaya ya Kibondo Taus Feruzi amesema kura za maoni zinafanyika jumamosi hii Machi 27 mwaka huu baada ya siku mbili za kuchukua na kurejesha fomu.

Bwana Feruzi amesema Wagombea wote wamepewa maelekezo ya kufanya ikiwa ni pamoja na kujiepusha na vitendo vya  rushwa na atakayebainika hatua za kinidhamu zitachukuliwa dhidi yake.

Tume ya Taifa ya uchaguzi kupitia kwa Mkurugenzi mkuu wa uchaguzi Dk.Wilson Mhera imetoa ratiba ya uchaguzi ikionyesha kuwa wagombea kupitia vyama mbalimbali vya siasa watachukua fomu kwa msimamizi wa uchaguzi tarehe 28 machi hadi tarehe 3 April ambayo pia itakuwa ndio siku ya uteuzi wa wagombea.

Kampeni za uchaguzi huo zitaanza April 4 hadi mei mosi na uchaguzi utafanyika Mei 2, 2021 mwaka huu.

 

 Source : Itv

Share To:

Post A Comment: