Na. Edward Kondela
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Pauline Gekul amesema kwa kushirikiana na Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki wameanza kufanya kazi kwa kasi kubwa ili kufahamu vipaumbele vya wizara hiyo, ambavyo vinapaswa kujumuishwa katika bunge la bajeti kwa mwaka wa fedha 2021/22.

Akizungumza mjini Arusha mwishoni mwa wiki (12.12.2020) na baadhi ya watumishi wa Kituo cha Taifa cha Uhilimilishaji (NAIC) mara baada ya kufanya ziara ya kikazi katika kituo hicho, Mhe. Gekul amesema kwa kufanya hivyo itakuwa rahisi kwao kumshauri Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Magufuli kwa mambo ambayo yatakuwa na tija kwa taifa na kuyapa vipaumbele.

“Tunakimbia kasi ili tunapoelekea kwenye bajeti tuweke vitu vyenye kipaumbele kwamba sasa kwa jinsi sekta hii inavyokwenda tutakuwa kwenye nafasi pia ya kumshauri mheshimiwa rais kwamba tunachoona sasa kinavyoendelea hiki hakikubaliki na hiki kingine kinakubalika na tunadhani tukipe kipaumbele ili mwisho wa siku mambo yaende vizuri.” Amesema Mhe. Gekul

Aidha, Mhe. Gekul amewataka wafanyakazi hao kufanya kazi kwa bidii na kutoendekeza uzembe huku akivitaka vitengo vya masoko na kukusanyia takwimu vya kituo cha NAIC kuongeza mawasiliano ili kutoa taarifa za mbegu za ng’ombe bora zinazozalishwa katika kituo hicho ili kufahamu namna mbegu hizo zinavyoleta tija na namna wafugaji wanavyozipokea na pia kufahamu matokeo yake.

Pia, amesema kwa kufanya hivyo kutasaidia kuboresha utendaji kazi wa kituo na kuonekana kwa matokeo chanya kwa uzalishaji wa mbegu hizo ili zilete tija na kuboresha maisha ya watanzania, wafugaji na kukuza pato la taifa.

“Pale tunapohitaji mpaboreshe ndugu zangu naomba mpaboreshe mheshimiwa rais wetu ana imani kubwa sana na nyinyi wataalamu kwa sababu ndiyo mnaotekeleza ilani kwa vitendo, niwaombe hili la masoko mlifanyie kazi kubwa sana hili likishafanyika hata uzalishaji utaongezeka, tutakuza uchumi wetu, tutatoa ajira na maisha ya watanzania yatakuwa yameboreka.” Amefafanua Mhe. Gekul

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Huduma za Mifugo kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Hezron Nonga amemwambia naibu waziri huyo kuwa kwa sasa kituo cha NAIC kinazalisha zaidi mbegu bora za ng’ombe kuliko idadi ya mbegu zinazopelekwa sokoni.

Ameongeza ni wakati sasa kwa kituo hicho kuhakikisha wanatumia vyema madume ya mbegu ambayo yamenunuliwa kwa gharama kubwa na serikali kwa ajili ya kuzalisha mbegu ambazo zimekuwa zikiwekwa kwenye mji wa mimba wa ng’ombe jike kwa njia ya uhimilishaji ili kuboresha kosaafu za ng’ombe.

Prof. Nonga amefafanua kuwa kwa sasa kituo cha NAIC kimekuwa kikijiendesha kwa gharama kubwa ilhali hakipeleki mbegu nyingi sokoni kutokana na uhitaji mdogo, ambapo amesema agizo la Mhe. Gekul la kuimarishwa kwa vitengo vya masoko na kukusanyia takwimu vya kituo hicho ni muhimu ili kuwafikia wahitaji wengi wa mbegu hizo na kutoa elimu.

Awali akitoa taarifa fupi ya kituo cha NAIC kwa Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Pauline Gekul, Mkurugenzi wa kituo hicho Dkt. Paul Mollel amesema kituo kimefanikiwa kusambaza mbegu bora za ng’ombe sehemu mbalimbali za nchi kuanzia Mwaka 2016 hadi sasa walau dozi Elfu 30 hadi Elfu 50, ambapo mikoa inayochukua mbegu nyingi ni Kilimanjaro na Arusha akitolea mfano kwa mwaka 2019 Arusha ilichukua takriban dozi Elfu 12 na Mkoa wa Kilimanjaro dozi Elfu Tatu huku mikoa mingine ikichukua kidogo.

Katika ziara hiyo ya siku moja Mkoani Arusha, Naibu Waziri Gekul ametembelea pia Kampuni ya Shazain inayohusika na ufugaji wa samaki na na uzalishaji wa vifaranga vya samaki ambapo amesema kwa sasa wizara inawekeza katika ufugaji wa samaki ikilenga azma ya serikali ya awamu ya tano katika kipindi cha miaka mitano ijayo kutoa ajira Elfu 45 kupitia ufugaji huo.

Mhe. Gekul amemtaka Mkurugenzi wa kampuni hiyo Bw. ZainaAli Bhimani kuendelea kushirikiana na wizara pia kuwasaidia wafugaji wadogo elimu juu ya ufugaji wa samaki ili watanzania wengi waweze kujitokeza kufuga na hatimaye taifa kuwa na mazao mengi ya samaki yanayotokana na ufugaji ili kutosheleza hitaji la taifa la ongezeko la samaki wa kufuga na kutoa ajira.  

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Pauline Gekul amekuwa katika ziara za mwanzo katika maeneo yanayogusa sekta za mifugo na uvuvi, mara baada ya kuteuliwa na hatimaye kuapishwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Magufuli kushika wadhifa huo akimsaidia Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki.
Share To:

Post A Comment: