
Katibu
Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Prof. Elisante Ole Gabriel (Wa
pili kutoka kushoto) akiwa kwenye maombi mafupi ya kuliombea taifa dhidi
ya maambukizi ya Virusi vya Corona muda mfupi kabla ya kuanza kukagua
josho la mifugo lililopo mnada wa awali wa Buzirayombo uliopo Wilaya ya
Chato Mkoa wa Geita leo.

Katibu
Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Prof. Elisante Ole Gabriel
(kulia) akizungumza na baadhi ya watendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya
Chato na wakala wa majengo (TBA) leo kwenye eneo la mnada wa wa awali wa
Buzirayombo unapotarajiwa kufanyika ujenzi wa majengo ya kisasa ya
mnada wa upili .

Mkurugenzi
Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Chato Bw. Leonard Mwaisabula
akielezea manufaa ya mnada wa upili wa Buzirayombo kwa upande wa
halmashauri hiyo pindi utakapoanza kazi wakati wa ziara ya Katibu Mkuu
Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Prof. Elisante Ole Gabriel leo
alipofika Wilayani humo kwa ajili ya kukagua eneo itakapojengwa
miundombinu ya mnada huo.

Meneja
wa Wakala wa Majengo (TBA) Mkoa wa Geita Mhandisi Gladys Jeffa mapema
leo akifafanua hatua ambazo mpaka sasa ofisi yake imefikia kabla ya
kuanza ujenzi wa miundombinu ya mnada wa Upili wa Buzirayombo
unaotarajiwa kuanza kabla ya mwezi Julai mwaka huu.

Katibu
Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Prof. Elisante Ole Gabriel
(katikati), Meneja wa Wakala wa Majengo (TBA) mkoa wa Geita Mhandisi
Gladys Jeffa (kushoto) na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya
ya Chato Bw. Leonard Mwaisabula wakielekea kwenye josho la mifugo
lililopo ndani ya mnada wa awali wa Buzirayombo wakati wa ziara yake ya
kukagua eneo hilo la mnada leo

Katibu
Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Prof. Elisante Ole Gabriel
(kushoto) akipokea maelezo ya namna utakavyokuwa mnada wa Upili wa
Buzirayombo baada ya kukamilika kwake kutoka kwa Mhandisi wa Wakala wa
Majengo (TBA) Bw. David Luoga leo alipofika kwenye eneo hilo kwa ajili
ya kukagua.

Katibu
Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Prof. Elisante Ole Gabriel
akisoma maelezo ya kibao cha ufunguzi wa kliniki ya Mifugo iliyopo
Wilayani Chato ambako alifika leo kwa ajili ya kukagua miundombinu ya
kliniki hiyo inayotarajiwa kukarabatiwa upya kwa ushirikiano baina ya
Halmashauri ya Wilaya hiyo na Wizara ya Mifugo na Uvuvi.
........................................................................................
Na.Mwaandishi wetu,Chato
Katibu
Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Prof. Elisante Ole Gabriel
amewataka wataalam wa sekta ya mifugo kote nchini watumie muda mwingi
kwenda kuwahudumia wafugaji badala ya kukaa ofisini.
Prof.
Ole Gabriel ameyasema hayo mara baada ya kufika kukagua moja ya kliniki
za mifugo iliyopo Wilaya ya Chato Mkoani Geita leo ambapo amemshauri
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya hiyo Bw. Leonard Mwaisabula kutenga
kiasi cha fedha cha kuanza ukarabati wa kliniki hiyo na Wizara yake
itamuunga mkono kwa kukamilisha hatua zilizobaki.
"Ni
kweli Wizara ina mpango wa kukarabati kliniki zote za Mifugo hapa
nchini lakini kipaumbele chetu cha kwanza ni kwa zile halmashauri ambazo
zitakuwa zimeshaanza ukarabati kwa kutumia fedha za mapato yao ya ndani
hivyo kama Chato mkianza mapema Wizara pia itawapa kipaumbele na
hatimaye muwe mfano kwa wengine" Aliongeza Prof. Ole Gabriel.
Kwa
upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Chato Bw. Leonard
Mwaisabula amesema kuwa halmashauri yake itayafanyia kazi ushauri huo
kwa sababu wana shauku kubwa ya kuona kliniki hiyo inafanya kazi.
"Nimepokea
ushauri wako Mhe. Katibu Mkuu na kesho tutakutana kwa ajili ya
kuangalia mchanganuo wa fedha tulizokuwa tumetenga kwenye idara ya
mifugo ili kuona namna tunavyoweza kuanza na ukarabati wa kliniki hii
kwa sababu kwetu ina umuhimu Mkubwa sana" Alisema Bw. Mwaisabula.
Mara
baada ya kutoka kwenye eneo hilo Prof. Olr Gabriel alielekea kwenye
eneo la mnada wa Buzirayombo unapotarajiwa kujengwa mnada mkubwa wa
upili ambako alioneshwa kuridhishwa na usanifu wa michoro inayoonesha
namna mnada huo utakavyokuwa baada ya kukamilika kwake.
"Lakini
pia nimeona eneo hili la mnada litakuwa linajumuisha pande mbili
zinazotenganishwa na barabara hivyo Mkurugenzi kwa kushirikiana na
Wakala wa Majengo (TBA) ni lazima muangalie namna ya kufanya ili
kuhakikisha wananchi wanakuwa salama wakati wote wakiwa kwenye eneo la
mnada" Aliongeza Prof. Ole Gabriel.
Pia
alipendekeza kutokana na michoro ya mnada huo kuonesha ni wa kisasa ni
lazima kuwe na mfumo mzuri wa matangazo ndani ya eneo la mnada, kituo
kizuri cha Polisi kitakachofanya kazi kwa saa 24, Mfumo wa kibenki na
huduma za afya zitakazowanufaisha wananchi wote watakaokuwa karibu na
eneo hilo la mnada, Runinga kubwa itakayoonesha kila kinachoendelea
Mnadani hapo na mfumo mzuri wa kuhifadhi idadi na aina ya bidhaa na
huduma zinazopatikana mnadani hapo ili kuwe na utaratibu wa kupata
taarifa zote muhimu ndani ya muda mfupi.
Kwa
upande wake Meneja wa TBA Mkoa wa Geita Mhandisi Gladys Jeffa
aliishukuru Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa ushirikiano Mkubwa
iliowaonesha mpaka sasa ambapo aliahidi kufanya kazi nzuri
itakayokamilika kwa wakati.
"Tunataka
kuhakikisha mpaka kufika mwisho wa Mwezi Mei tuwe tumekamilisha na
kuwasilisha hii hatua ya michoro yote ya mnada huu na tunataka kabla ya
kuvuka mwaka huu wa fedha mkandarasi awe site" Alisisitiza Mhandisi
Jeffa.
Naye
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Chato Bw. Leonard
Mwaisabula alisema mradi huo kwao una manufaa makubwa kwa sababu
utaongeza kiasi cha makusanyo ya fedha za ndani na hivyo kuiwezesha
Halmashauri kuboresha miundombinu ya huduma mbalimbali za jamii kama
vile Elimu na afya.
Post A Comment: