
Kaimu
Meneja Mkuu wa hifadhi ya ranchi za taifa (NARCO) CPA Masele Mipawa
akitoa ufafanuzi juu ya namna walivyoanza kutekeleza agizo la kuweka
alama za kuonekana kwenye ranchi hizo wakati wa kikao baina ya Katibu
Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Prof. Elisante Ole Gabriel,
viongozi wa Wilaya ya Muleba na timu ya wataalam wanaoendelea na zoezi
la kurekebisha ramani ya ranchi ya Mwisa II leo.

Katibu
Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) (Katikati) Prof. Elisante Ole
Gabriel akiwa kwenye picha ya pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa
Halmashauri ya Wilaya ya Muleba Bw. Emmanuel Shelembi (Kushoto), Mkuu wa
Wilaya ya Muleba Mhe. Mhandisi Richard Ruyango leo (18.04.2020) huku
wakitekeleza agizo la Wizara ya afya, la kusimama mita moja baina ya mtu
mmoja na mwingine ili kuepuka maambukizi ya virusi vya Corona.

Katibu
Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) (Katikati) Prof. Elisante Ole
Gabriel akiwa kwenye picha ya pamoja na timu ya wataalam wanaoendelea na
zoezi la kurekebisha ramani ya ranchi ya Mwisa II muda mfupi baada ya
kumalizika kikao baina yao leo
...................................................................................
Na.Mwaandishi Wetu,Muleba
Katibu
Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Prof. Elisante Ole Gabriel
ameitaka hifadhi ya ranchi za taifa (NARCO) kwa kushirikiana wadau
wengine wa sekta ya Mifugo kuhakikisha Nchi inakuwa na Mifugo ya kutosha
na yenye afya kwa ajili ya kukidhi mahitaji ya bidhaa zitokanazo na
mifugo wakati huu wa janga la Ugonjwa wa homa kali ya mapafu
unaosababishwa na virusi vya Corona (Covid 19) na hata mara baada ya
janga hilo kuisha.
Prof.
Elisante Ole Gabriel aliyasema hayo mapema leo alipofanya ziara katika
Wilaya ya Muleba mkoani Kagera lengo likiwa ni kukagua utekelezaji
marekebisho ya upimaji wa ramani ya Ranchi ya Mwisa II ili kutenga eneo
lililopendekezwa kuhamishia wananchi waishio ndani ya Ranchi hiyo.
"Wakati
huu wa hili janga la Corona mahitaji ya nyama Afrika na duniani ni
makubwa sana na yanaweza kuongezeka maradufu mara baada ya janga hili
kuisha hivyo ni lazima tujipange ili kuhakikisha tunakuwa kitovu cha
usambazaji wa bidhaa zitokanazo na mifugo duniani na NARCO mnapaswa
kujitokeza kifua mbele kuwa hilo mnaliweza na lipo ndani ya uwezo wenu"
Aliongezea Prof. Ole Gabriel.
Alisisitiza
katika kutekeleza hilo NARCO wanapaswa kutafakari vizuri na kuchagua
ranchi moja ya kimkakati kati ya 14 zilizopo hapa nchini ambayo
watawekeza kwa dhati ili waweze kunenepesha ng'ombe wengi
watakaosafirishwa nje ya nchi zenye mahitaji makubwa ya mifugo na bidhaa
zake kwa sasa.
"Lakini
pia katika kuelekea kwenye uchumi wa kati unaotegemea viwanda 2025 ni
lazima NARCO iainishe ranchi tano za mfano ambazo wananchi na wadau
mbalimbali watafika kwa ajili ya kujifunza juu ya ufugaji wa kisasa na
pia zitumike kama shule hata kwa wanaokodisha ranchi nyingine ili nao
wafike kujifunza namna ya ufugaji bora utakaolenga kuzalisha mifugo
itakayowawezesha kunufaika kiuchumi" Alisisitiza Prof.Ole Gabriel.
Awali
akisoma taarifa ya utekelezaji wa marekebisho ya upimaji wa ramani ya
Ranchi ya Mwisa II, kiongozi wa timu ya wataalam wanaofanya kazi hiyo
Bw. Fikiri Mwasenga alisema kuwa kazi hiyo inatarajiwa kukamilika ndani
ya siku 30 kuanzia hivi sasa na mpaka sasa tayari timu hiyo
imeshakamilisha kumega maeneo ya vitongoji vitatu ambavyo ni Butera,
Bionza na Rwenzige na kazi ya kupima maeneo mawili yaliyobaki inaendelea
ili kuweza kukamilisha maeneo yote matano yaliyopendekezwa kutengwa.
Kwa
upande wake Mkuu wa Wilaya ya Muleba Mhe. Mhandisi Richard Ruyango
aliishukuru Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa hatua yake ya upimaji wa
maeneo hayo ya ranchi ya Mwisa II kwani hatua hiyo itaondoa na kumaliza
kabisa migogoro iliyokuwepo baina ya wakulima na wafugaji waliopo kwenye
maeneo ya ranchi hiyo.
Ranchi
ya Mwisa II ni miongoni mwa ranchi 14 zilizopo chini ya hifadhi ya
ranchi za taifa (NARCO) ambapo ina ukubwa wa hekta 133,000 na inatajwa
kuwa ranchi kubwa kuliko zote hapa nchini.
Post A Comment: